![]() |
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam kujibu madai ya TEWUTA. |
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imepinga madai yaliyotolewa na Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) jana dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL na kufafanua kuwa madai hayo si ya kweli zaidi ya upotoshaji wenye nia ovu ya kufanikisha malengo binafsi na kutaka kuikwamisha jitihada za TTCL katika maendeleo.
Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari leo Makao Makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam alisema madai yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL hayana ukweli wowote bali wahusika walilenga kuupotosha umma.
"Menejimenti ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), inapenda kuujulisha Umma kuwa, madai yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL si sahihi. Hoja hizo zimejikita katika upotoshaji wenye nia ovu ya kufanikisha malengo binafsi ya wahusika na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye nia na malengo ya kutekeleza mpango mkakakti wa kuiboresha na kuiimarisha Kampuni ya Simu Tanzania.
Akifafanua zaidi Meneja Uhusiano huyo wa TTCL alisema mwaka 2007 Kampuni ya Simu Tanzania ilifanya mabadiliko ya Muundo wa Kampuni ili kuendana na hali ya soko la Ushindani katika sekta ya mawasiliano na Muundo uliopo sasa ni ule uliopitishwa na kuanza Kutumika mwaka 2007 baada ya kuidhinishwa na kupitishwa na Bodi ya Wakurugenzi.
Alisema menejimenti mpya ya TTCL iliyoanza kazi Februari 2013 iliainisha changamoto mbalimbali za kibiashara na kutengeneza Mpango Mkakati utakaoletab mabadiliko ya kibiashara na kuongeza tija, huku ikizingatia mabadiliko ya Kibiashara na ushindani wa soko katika sekta ya mawasiliano, Menejimenti iliomba na kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL kumtafuta Mshauri mwelekezi kwa njia ya Zabuni ili kupitia na Kushauri juu ya Muundo Mpya wa Kampuni utakaoendana na Mahitaji ya Kibiashara na kuleta ufanisi.
Aliongeza kuwa matokeo ya Kazi ya Mshauri mwelekezi yamelenga kubadilisha muundo wa Kampuni, Muundo wa Mishahara na Muundo wa utumishi. Mpango huu wa Mabadiliko ya Kibiashara unategemewa kukamilika katika kipindi cha mwaka 2016. Aidha alifafanua kuwa muundo wa mishahara unaotumika hivi sasa ni ule uliopitishwa Mwaka 2007 baada ya Kubadilika kwa Muundo wa Kampuni kama ulivyoidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL.
"...Mfumo huu uliiweka TTCL katika nafasi ya kukabiliana na soko la ajira kimaslahi. Mfumo huu wa Mishahara ulizingatia pia matakwa ya kisheria ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6/2004 zimeainishwa aina tatu za Mikataba ya Ajira. Yaani: Mkataba wa Ajira usiokuwa na Muda Maalumu (Unspecified period of time), Mkataba wa Ajira wa Muda Maalum (Fixed Employment contracts) na pia Mkataba wa Ajira wa kazi Maalum (Special Task)..."
"...Hivyo Muundo wa Mishahara uliopitishwa mwaka 2007 uliainisha madaraja ya malipo na viwango husika ikiainisha aina ya mkabata, Mkataba wa Ajira usiokuwa na Muda Maalum na Mkataba wa Ajira wa Muda Maalum. Katika muundo huu madaraja na ngazi za Mishahara zimegawanyika katika ngazi Kumi (10) kuanzia TTCL 1 (Ikiwa ndio Kiwango cha Juu) hadi TTCL 10 (Ikiwa ndio kiwango kidogo) Muundo huu uko wazi na ndio unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni ya Simu Tanzania. Hakuna ulipaji wa mishahara (Payroll) yoyote ya Siri inayotumika tofauti na hiyo iliyoainishwa," alifafanua Meneja Uhusiano huyo katika taarifa yake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...