Na Kaka Mwinyi
Msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Flava, Luteni Karama (kushoto),
amefanya ujio mpya wa kimuziki baada ya kuachia ngoma moja kali iitwayo ‘The
Way I Feel’ akimshirikisha msanii toka Ufaransa, Jerry Julian (chini) na tayari imeanza
kufanya vema kwenye mitandao na vituo vya redio na runinga.
Karama amepasha kuwa, baada ya kimya kirefu, ameamua kurejea
kwenye game kwa mtindo tofauti ambapo muelekeo wake unathibitika katika kazi
yake mpya ya The Way I Feel ambayo tayari imeshapakuliwa mara laki moja na
ushee tangu aiachie rasmi wiki tatu zilizopita.
“Nimeamua kuja kivingine. Si unajua siku hizi game
imebadilika sana. Lazima ujiongeze na kuangalia mwelekeo kabla hujafanya
chochote, ndio maana nikaamua kumshirikisha Jerry Julian ambaye kishafanya kazi
kwenye majukwaa makubwa ya Ulaya kama Paris, Amsterdam, London na Marekani ya
Kusini. Ukifungua Youtube utaiona na
utabaini ninamaanisha nini,” akasema Karama.
Msanii huyu aliyezikoga sifa kedekede akiwa na kundi la
Gangwe Mobb akiwa na mwenzake Inspektah Haroun, amesema kuwa, wimbo wake huo
umerekodiwa Natal Studio hapa nchini huku ukifanyiwa mixing nchini Ufaransa na studio ya 20K Records kisha mastering ikafanywa na Macles Studio ya
Ubelgiji ambayo wanamuziki wengi wa Reggae na Dancehall hufanyia kazi zao.
“Kwa kweli this time
around sijabahatisha, ninamaanisha ninachokifanya nan i mwanzo wa mfululizo
wa kazi nzuri siku za usoni. The Way I Feel imebeba mseto wa Bongo Flava na
mirindimo ya ki-Caribbean na baada ya kuachia kazi zingine tano nilizoandaa na
wasanii mbalimbali nitafanya ziara ya mataifa mbalimbali kwa mujibu wa ratiba
yangu,” akasema kwa kujinasibu.
Tayari wimbo huo umepata wasikilizaji wengi mitandaoni huku
wengine wakiupakua (downloading) kutoka mitandao ya YouTube, Facebook na blogu
mbalimbali maarufu kote nchini na baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani, hatua
ambayo Karama anadai inachagizwa na ubora wa video yake iliyotengezwa na Minzi
Mims wa Fine Image ya jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...