Na Tamimu Adam, Jeshi la
Polisi.
Jeshi la polisi nchini, limeanzisha
mpango wa kuboresha usalama wa
jamii nchi nzima ambao unalenga kuboresha
utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuboresha mawasiliano ya ndani na nje ya Jeshi la polisi kwa kuwashirikisha
wadau mbalimbali wa usalama
ambapo mpango
huo utaanza kutekelezwa katika mkoa wa kipolisi kinondoni ambapo lengo lake ni kupunguza uhalifu kwa asilimia kumi ifikapo
mwaka 2019.
Akihitimisha maabara ya mpango huo iliyofanya kazi kwa
wiki sita, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi
Abdulrahmani Kaniki (pichani) aliwahakikishia washiriki wa maabara ya kuboresha usalama wa
jamii, kuwa Jeshi la polisi litatekeleza
kwa vitendo mapendekezo yote yaliyotokana na maabara hiyo, kwani baadhi
ya mapendekezo hayahitaji bajeti hivyo utekelezaji wake utaanza mara moja.
“Kazi iliyofanywa na maabara hiyo ni kubwa na umuhimu katika kuboresha usalama wa jamii
katika nchi yetu hivyo mapendekezo yote ni lazima yafanyiwe kazi ili kuleta
mafanikio chanya”. Alisema Kaniki.
Aliongeza kuwa mpango huo umeanzia katika mkoa wa kipolisi kinondoni na baadaye
utaenea nchi nzima, ambapo alizitaja sababu zilizopelekea kuanza na kinondoni
kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa makosa, kupanuka mji, idadi kubwa ya watu na uwepo na
shughuli nyingi za kiuchumi ukilinganisha na maeneo mengine.
Naye, Mtendaji mkuu wa ofisi ya Rais ya ufuatiliaji wa utekelezaji
wa miradi (PDB), Omari Issa alisema mpango huo wa uboreshaji wa usalama wa jamii
ambao unaanza na mkoa wa Kinondoni uliandaliwa kwa kuwashirikisha wadau kutoka
taasisi mbalimbali za serikali na kijamii ambao kwa pamoja walishirikiana kwa
pamoja katika kuangalia namna ya kuboresha usalama wa jamii ili kuwezesha jamii kuwa salama.
Aliongeza kuwa mpango wa matokeo
makubwa sasa unahitaji kuzingatia vitu vikuu vitatu katika utekelezaji wake
ambavyo ni kujiwekea vipaumbele, nidhamu ya utekelezaji na uwajibikaji hivyo
alisema hana wasiwasi na Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa mpango huo hapa
nchini.
Mpango wa uboreshaji wa
usalama wa jamii unalenga kuboresha
na kurahisisha huduma mbalimbali zinazotolewa na Jeshi la polisi ikiwemo
kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa askari, usimamizi wa rasirimali watu
na vifaa na kuweka mikakati ya kuwashirikisha wadau wa kada mbalimbali
ndani ya jamii katika kuboresha usalama
wa jamii.
Maabara hiyo ya kuboresha usalama wa jamii ripoti yake
inatarajiwa kukabidhiwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi hivi karibuni ili
kuanza utekelezaji wake kwa kuanza na mkoa wa kipolisi wa Kinondoni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...