Na Jacquiline Mrisho -MAELEZO
Watanzania wameaswa kuzingatia Maadili ya Kitaifa ambayo ni kiini cha kuboresha na kusimamia maadili ya viongozi, watumishi wa Umma na watu wanaojishughulisha na sekta binafsi nchini ili kuendelea kuimarisha utendaji kazi na kupambana na uovu katika jamii.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mhe. Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo ambapo alisema kuwa maadili ya Taifa ni moja ya tunu muhimu zinazolitambulisha taifa na kutofautisha taifa moja na mataifa mengine.
“Maadili ya mtu binafsi au yaTaifa hayaoti kama uyoga, lazima yajengwe, yaendelezwe na yalindwe na watu waliodhamiria kufanya hivyo, siyo mara moja tu bali ni muendelezo” alisema Balozi Sefue.
Balozi Sefue ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha utendaji na kupambana na uovu katika jamii hususani rushwa na utovu wa nidhamu na ambapo Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa watumishi wa umma wanaotumia nafasi zao kujitajirisha na kujilimbikizia mali kwa njia zisizo halali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Roundtable, Bw. Ali Mufuruki aliunga mkono hotuba ya Mhe. Balozi Sefue kwa kusema kuwa hafikirii polisi au nguvu ya Mhe. Rais peke yake itaweza kuzuia uvunjifu wa maadili bali wananchi wote wanatakiwa kushiriki katika kuzuia uvunjifu huo wa maadili.
Maadhimisho ya Maadili ya Taifa kwa Tanzania huazimishwa kila mwaka Desemba 10 kwa kuwa Desemba 09 Tanzania Bara huadhimisha sikuu ya Uhuru, chimbuko la sherehe hiyo ni kumbukumbu ya vita dhidi ya rushwa ambayo hufanyika Desemba 09 kwa nchi zote duniani.
Maadhimisho hayo yameambatana na majadiliano yaliyoshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Taasisi za Umma, Wafanyabiashara, Muwakilishi kutoka USAID Bi Frola Henjewele, Wawakilishi kutoka Sekta Binafsi, Taasisi za Kiraia,Viongozi wa Dini pamoja na Wanafunzi kutoka Vyuo na Shule mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...