Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande amewataka Mawakili kote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma ya Sheria na kwamba wasisite kuwaeleza ukweli wateja wao wanaopeleka mashauri Mahakamani ili kuepuka kupoteza muda na gharama katika masuala yanayoweza kupatiwa ufumbuzi nje ya Mahakama.
Akizungumza na Mawakili wapya 104 waliohitimu Shule ya Sheria kwa mwaka 2015 wakati wa hafla ya 53 ya kuwapokea na kuwaapisha iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee leo jijini Dar es salaam amesema kuwa msingi mkubwa wa kazi yao umejengwa katika uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya sheria.
Amewataka Mawakili hao kubadilika kifikra kwa kuwa Mawakili Bora ili kujenga imani na uaminifu kwa jamii wanayoihudumia na kuongeza kuwa
sasa wameingia kwenye utaratibu wa kutambuliwa rasmi na Mahakama ya Tanzania kwa kuwezeshwa kufanya shughuli za uwakili kwenye mahakama ya Tanzania maeneo mbalimbali nchini.
“Naomba mtambue kuwa kila Wakili ni Ofisa wa Mahakama hivyo mnao wajibu na jukumu la kusoma, kufuatilia mashauri mbalimbali ili kuwa na uhakika wa kesi mnazosimamia kuliko kuzitegemea Mahakama”
Aidha, ameeleza kuwa yapo mambo ambayo yamekua yakifanywa na baadhi ya Mawakili wasio waaminifu yanayochafua sura ya Taaluma ya Sheria ikiwemo kutumia nyaraka za kughushi, kuvunja Kanuni na Maadili ya Taaluma huku baadhi yao wakijikuta wakiingia katika mgogoro na Mamlaka zinazosimamia kitaaluma taaluma hiyo.
“Nawataka mzingatie sheria, kanuni na Maadili ya Uwakili, hata hivyo tuna chombo kinachosimamia maadili yenu, wapo takribani 176 waliokiuka maadili na hawa wanashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ili kulinda maadili na utendaji wa taluma yenu” Amesisitiza Mhe. Othman.
Amewataka watimize wajibu wao kwanza kwa wananchi watakaouhudumia pamoja na Mahakama ya Tanzania ambayo inawataka kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Mhe. Othman amefafanua kuwa Mahakama ya Tanzania inaendelea na Mkakati wa kupunguza mrundikano wa Kesi Mahakamani kwa kuhakikisha kuwa kesi zote zinazofikishwa Mahakamani zinamalizika katika kipindi cha chini ya mwaka 1
Ameeleza kuwa silimia 47 ya kesi zaidi ya 200 zilizokuwepo Mahakama Kuu katika kipindi cha miaka 4 iliyopita zimeendelea kusisikilizwa kwa ubora na sasa zimebaki asilimia 17 ya kesi hizo jambo linaonyesha kuongezeka kwa ufanisi wa Mahakama.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju akiwakaribisha Mawakili hao katika familia ya sheria Tanzania amesema kuwa katika jamii wanao mchango mkubwa katika kuhakikisha Haki na Usawa vinadumishwa nchini.
Amesema mawakili hao kabla ya kuapishwa na kuingizwa kwenye utaratibu wa kutambuliwa kuwa Mawakili wamepitia na kufauru vigezo vya kitaaluma vilivyowekwa ili kulinda heshima ya Taaluma ya sheria nchini.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande akiongoza
maandamano ya Majaji na Watendaji wa Mahakama wakati wa hafla ya 53 ya
kuwapokea na kuwaapisha Mawakili wapya 104 iliyofanyika katika viwanja vya
Karimjee leo jijini Dar es salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande akizungumza
na Mawakili 104 walioapishwa leo jijini Dar es salaam. Mhe. Chande amewataka
Mawakili hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma yao.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande (katikati)
akiongoza akiwa na Majaji na Watendaji wa Mahakama wakiendelea na zoezi zoezi
la kuwaapisha Mawakili wapya 104 katika viwanja vya Karimjee leo jijini Dar es
salaam.
. Mawakili wakiwa wamesimama mbele ya Jaji Mkuu kabla
ya kuapishwa.
Mawakili walioapishwa wakiwa katika picha ya pamoja na
Jaji Mkuu Mhe. Othman Chande na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania.
Picha na Aaron Msigwa –MAELEZO.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...