MRADI wa Mabasi yaendayo haraka (BRT) kuanza Januari 10, 2016 hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa wakati akikagua ujenzi wa miundo mbinu ya Mradi wa Mabasi yaendayo haraka leo jijini Dar es Salaam.
Pia Majaliwa amewaagiza watendaji wizara ya Tamisemi ambao ni wamiliki wa mradi huo kusimamia vyema ili uanze kufanya kazi kama ilivyo pangwa kwa kuwa mabasi 120 yalishawasili jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ameanza kwa kukagua vituo vya mradi huo kuanzia cha Feri, Jangwani, Kimara na kumalizia na Morocco na kuwapongeza kwa kumaliza kujenga vituo 15 kati ya 27 na amewaagiza kumalizia vituo vilivyo baki ili kufikia januari 10 mwakani mabasi yaanze kufanya kazi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na watendaqji mbalimbali wa mradi wa mabasi yaendayo haraka waliofika katika kituo cha Feri cha Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (BRT) leo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akitembelea maeneo mbalimbali ya kituo cha Feri jijini Dar es Salaam leo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akipanda basi la mwendo wa haraka mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali katika kituo cha feri leo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa katika kituo cha Mradi wa mabasi cha Jangwani kukagua maendeleo ya ujenzi ya kituo hicho ikiwa ujenzi wa kituo hicho upo hatua za mwisho kukamilika.
Picha na Avila Kakingo wa Globu ya Jamii.
KWA PICHA ZAIDI BOFYA HAPA.
WAZIRI MKUU AKAGUA MIUNDOMBINU YA DART
· Ataka ianze kazi Januari 10, mwakani kama walivyoahidi
· Aanzia Feri - Kimara na kumalizia Magomeni – Morocco
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) na wadau wote kuhakikisha kuwa mradi huo unaanza kufanya kazi ifikapo Januari 10, 2016 kama walivyokubaliana kwenye kikao cha Novemba 27, 2015.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Desemba 19, 2015) wakati akizungumza na viongozi wa TAMISEMI, TANROADS, watendaji wa mradi huo, viongozi wa mkoa na Manispaa ya Kinondoni mara baada ya kumaliza kukagua mradi huo katika eneo la Morroco, jijini Dar es Salaam.
“Nataka kusisitiza kuwa ahadi ya kuanza kutoa tarehe 10 Januari 2016 iko palepale. Fanyeni mapitio na mwendeshaji wenu mjiridhishe juu ya vipengele vyote vya mkataba. Badilisheni tiles za pale Feri kwa sababu mlishaambiwa kwamba ziko chini ya kiwango na mkakubali,” alisema.
Kuhusu moshi unaotoka kwenye soko la samaki la Feri, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa Jiji la Dar es Salaam wasimamie suala hilo kwa sababu Manispaa ya Ilala (ambao wanasimamia soko hilo) wako chini yao. “Mlisema mtabadilisha mfumo wa majiko lakini naona hakuna kilichofanyika. Nitakapokuja kukagua tena mradi huu mwisho wa mwezi, nitapita Feri kuona kama mmetekeleza agizo hilo,” aliongeza.
“Na hapa hamna jinsi, ama mbadilishe mfumo wenu wa majiko muweke yasiyotumia kuni na kutoa moshi kiasi kile au mtafute mahali pengine pa kuhamishia hilo soko ili watu waendelee na biashara zao,” alisema.
Amewataka wanasheria wa ofisi zote zinahusika na mradi huo wahakikishe kuwa wanasimamia mikataba na kuipitia upya ili wamiliki wa daladala ambao ni wadau wakuu wa mradi huo nao pia wasiachwe wakati mradi unaanza.
“Mwendeshaji wa UDART ambaye anaungana na waendeshaji wa daladala hakikisheni wanaingia kwenye mpango huo bila malalamiko. Wenye daladala ni watu ambao tumewatoa kwenye route zao, simamieni mikataba hii ili kusiwe na malalamiko yoyote juu ya umiliki,” alisema.
Alisema watoa huduma za uendeshaji ni lazima wafanye kazi sambamba na Serikali kwani ndiye mdau mkuu. DART ni wakala wa Serikali lakini UDART (UDA Rapid Transport) ni kampuni ya binafsi inayotoa huduma za mpito katika miundombinu ya DART. Huduma hizo ni pamoja na mabasi yanayotoa huduma, ukataji wa tiketi na huduma za ujazaji salio kwenye tiketi hizo.
UDART inamilikiwa kwa pamoja na shirika la UDA pamoja na muunganiko wa wamiliki wa Daladala ambao hadi sasa kuna DARCOBOA na UWADAR.
Waziri Mkuu alifanya ukaguzi wa miundombinu ya DART Kuanzia Feri hadi Kimara na kurudi kisha akaanzia Magomeni hadi Morocco. Pia alikagua depot ya mabasi ya mradi iliyopo Jangwani na kuridhika na hatua ambazo zimechukuliwa hadi sasa. Alikuwa akifuatilia utekelezaji wa maagizo aliyowapa Novemba 27, mwaka huu kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwake. Ameahidi kurudi na kukagua tena mradi huo mwishoni mwa mwezi huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...