Benki ya Posta Tanzania imetoa mikopo ya jumla ya million 244,500,000.00 kwa wajasiriamali 185 kwa ajili ya kukuza shughuli zao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mikopo hii imedhaminiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bi. Anna Dominick, amewambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa wajasiriamali hao 185 ni wanachama wa vicoba vinane.
“Kati yao wanawake 137 sawa na asilimia 74 na wanaume 48 sawa na asilimia 26,” na mkopo huu ni matokeo ya makubaliano kati baraza na benki yaliyofikiwa julai 14, 2015,alisema Bi. Dominick.
Amesema utoaji wa mikopo hii ni utekelezaji wa makubaliano ya Julai mwaka jana umeanza kwa kunufaisha baadhi ya vicoba katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, na kuongeza “huu ni mwanzo tu. Tutahudumia wajasiriamali wanaokidhi vigezo nchi nzima.
”
Vikundi vya vicoba vivilivyopata mikopo hiyo alivitaja kuwa ni Juhudi, Tayeeo Vicoba, Mwanga, Maendeleo, Mzingira, Umoja ni Nguvu, Gosofu na Nyota Njema.
Bi Dominick ameeleza kuwa makubaliano kati ya baraza na benki yanalenga kwenye kuwawezesha wananchi ili kukabiliana na tatizo la ajira nchini na kuongeza kwamba vicoba ni taasisi ndogo za kifedha zinazofanya kazi nzuri katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi Kuu ya Takwimu ya Taifa ya mwaka 2011 inakadiriwa vijana 800,000 hadi milioni moja wanapigania nafasi za ajira 60,000 katika sekta ya umma na 300,000 katika sekta binafsi
Bi. Dominick amesema kwa takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba kiasi cha vijana kati ya 400,000 hadi 600,000 wanakuwa hawana ajira katika soko la ajira kila mwaka.
“Hii ndiyo sababu tunayapa uzito mkubwa makubaliano haya kati ya baraza na benki.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania, Bw. Sabasaba Moshingi, amevisifu vikundi vya kijasiriamali vya vicoba na kueleza kwamba mikopo kwa vikundi hivi jambo la msingi katika vita dhidi ya hali duni ya maisha katika jamii.
“Benki hii imeweka kipaumbele katika kuwawezesha wananchi kiuchumi na mikopo inayotolewa ni ya riba nafuu ya asilimia 11. Tunaamini mikopo hii itazifanya shughuli za kijasiriamali kuendelea zaidi,alieleza Bw. Moshingi.
Bw. Moshingi amesema vicoba na vikundi vingine vijenge utamaduni kuweka akiba na kuanzisha shughuli za kijasiriamali na kurejesha mikopo kwa wakati ili vikope tena na kutoa nafasi ya wateja wengine kukopa.
Alisema baraza na benki ni vyombo vya serikali na kwamba mikopo inalenga kukinua wananchi na ili waweze kuinuka kiuchumi na kuchangia uchumi.
Mwenyekiti wa Nyota Njema,Bi. Pili Yomba, ambaye kikundi chao kiko Tandika Temeke alisema watatumia mkopo waliopata kukuza mtaji na kulipa marejesho kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania, Bw. Sabasaba Moshingi (kulia), anafafanua jambo wakati hafla ya kuwakabidhi mikopo wananchama wa vikundi vinanne vya vicoba ambavyo wananchama wake wametimiza sifa za kupata mikopo. Mikopo hiyo imedhaminiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), (Kushoto) ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bi. Anna Dominick.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania, Bw. Sabasaba Moshingi (kushoto) akimkabidhi hundi Mkurugenzi wa TYEEO, Bw. Ayubu Luhunga (kulia). TYEEO ni kati ya vikundi vinnane vilivyofuzu kupata mikopo ambayo imedhaminiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC. (Katikati) ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bi. Anna Dominick.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...