Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) iko mbioni kuanza kutumia Nguzo za kusambazia Umeme za Zege ili kuondokana na nguzo za miti ambazo zina changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kuvunjika, kuoza kwa kuliwa na wadudu na kuanguka hivyo kusababisha usumbufu kwa wananchi kukosa huduma muhimu ya umeme.

Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo alipokutana na Ujumbe kutoka Ujerumani Ofisini kwake hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Ujumbe huo uliongozwa na Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke ulimtembelea Mhandisi Chambo kwa nia ya kuwasilisha maombi ya kuwekeza katika sekta ya nishati kupitia mradi wa kujenga nguzo za kusambazia umeme za zege.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo Balozi Kochanke alisema endapo maombi yao yatakubaliwa, watatoa ajira kwa wazawa na kuwajengea uwezo ili waweze kuendeleza mradi huo pindi watalaamu hao watakapomaliza mkataba na kurejea kwao.

Katibu Mkuu Chambo alisema, “Ni vizuri tukaondokana na teknolojia ya zamani ya kutumia nguzo za kusambazia umeme za miti na kuhamia teknolojia ya kisasa ya nguzo za zege ambayo inatumika nchi mbalimbali zikiwemo za Umoja wa Ulaya na Mashariki ya Kati kama vile nchi ya Oman ambao kwa sasa tayari wanatumia nguzo za zege.

Aliongeza kuwa ni muhimu kuzigatia taratibu za manunuzi serikalini katika kuchagua Kampuni zenye sifa stahiki zinazojumuisha wawekezaji Wazawa na waotoka Nje ya nchi kwa ajili ya kazi ya kutengeneza nguzo hizo.

Akizungumzia faida za kutumia nguzo za zege Mhandisi Chambo alisema, “Nguzo zinazojengwa kwa kutumia zege ni imara na uhai wake ni zaidi ya miaka 100, ukilinganisha na nguzo za miti ambazo uhai wake hauzidi miaka 20 hali inayochangia matumizi ya nguzo za miti kuwa na gharama kubwa.

Kwa upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji na Huduma kwa Wateja Kutoka Tanesco, Mhandisi Sophia Mgonja alisema wakati mwingine Tanesco hulazimika kukata umeme kwa lengo la kubadilisha nguzo ambazo zinakuwa zimeoza na hali inayosababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi na kuingia gharama kubwa.

Aidha, Mgonja alisema kuwa Tanesco inategemea kuanza kutumia nguzo za zege baada ya kumaliza maandalizi yote muhimu na kwamba ni matumaini yake kuwa ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2016 watakuwa wamefikia hatua nzuri.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (mbele) na Ujumbe kutoka Ujerumani wakiongozwa na Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke (watatu kulia) wakiwa ofisini kwa Katibu Mkuu jijini Dar es Salaam kuwasilisha maombi yao ya kuwekeza katika ujenzi wa nguzo za kusambazia umeme za zege.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo akiwa amesimama kuangalia mfano wa Nguzo za kusambazia Umeme za Zege, katika kikao kilichofanyika ofisini kwake na Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke akiwa anamwonesha mfano huo wa nguzo wanazojenga. Katikati ni Naibu Balonzi wa Ujerumani, John Reyels.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (mbele), Naibu Balonzi wa Ujerumani inchin, John Reyels (Kulia kwa Mhandisi Chambo), Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke (wa tatu kulia) na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji na Huduma kwa Wateja Kutoka Tanesco, Mhandisi Sophia Mgonja akiwa anawafafanulia jambo katika kikao hicho.
Na Rhoda James

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. The mdudu, hii ni habari njema kwetu watanzania na nyie Tanesco tokeni kwenye mwendo wa kinyonga haya mambo ya eti ikifika 2016 tutakua tumefikia pazuri serikali ya awamu ya 5 chini ya Rais Magufuli hatutaki kusikia hizo kauli sisi tunachotaka kuona zinazalishwa hata kabla ya 2016 stop mambo ya tuko kwenye mchakato mala upembuzi yakinifu hayo maneno ndio yanayo ludisha kasi ya maendeleo nyuma so stop saying that please.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...