Katika kuitikia wito wa Raisi wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wa kusherekea siku ya Uhuru wa miaka 54 ya Tanzania, Taasisi ya Benjamin William Mkapa (The Benjamin William Mkapa Foundation- BMF) imeshiriki kikamilifu katika shughuli za usafi zilizofanyika siku ya maadhimisho ya Uhuru tarehe 9 desemba mwaka huu wa 2015 kwa kufanya usafi katika Zahanati ya Kawe iliyopo Manispaa ya Kinondoni, Dar Es Salaam.

Zoezi hili la usafi lilishirikisha wafanyakazi wa Taasisi pamoja na Diwani wa Kata ya Kawe, Mwenyekiti wa Serikali za mitaa Kawe na wajumbe wa bodi ya zahanati, ambao kwa pamoja walishirikiana katika kufanya usafi maeneo yote ya ndani ya jengo la zahanati pamoja na yanayoizunguka.

Taasisi ilichagua zahanati hiyo kufanyia usafi kutokana na ofisi ya Taasisi kuwa katika eneo la Kawe na pia kutokana na ushirikiano madhubuti ulipo kati ya uongozi wa Kata ya Kawe na Taasisi hii.
Bw. Issuja Kilian na Paul Mhakalira watumishi wa Taasisi ya BMF wakiwa katika shughuli ya usafi Zahanati ya kawe.

Akiishukuru Taasisi ya Mkapa, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kawe alisema, “Nashukuru Taasisi ya Mkapa kwa kujitolea kufanya usafi katika eneo letu, mmetupa mwamko mkubwa sana, na kwahiyo zahanati yetu kuanzia leo tutakuwa na utaratibu mpya wa kufanya usafi mkubwa angalau mara moja kwa mwezi kama mlivyofanya siku hii ya leo”
Mkurugenzi wa Programu wa Taasisi ya BMF, Bi Rahel Sheiza akifanya usafi katika Zahanati ya kawe.
Aidha, Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu kutoka Taasisi ya Mkapa, Bi Irene Ungani-Kyara alishukuru uongozi wa zahanati kwa kukubali ombi la Taasisi la kufanya usafi katika zahanati ya Kawe. Alisema usafi uliofanyika ulijumuisha sehemu zote za nje na ndani ya majengo ya zahanati hiyo ikiwemo mapokezi, vyumba vya kuchunguzia wagonjwa, maabara, wodi za kulaza wagonjwa, stoo, vyoo vya wafanyakazi na wagonjwa, pamoja na eneo la wazi lilioko nje ya majengo ya zahanati.

Bi Irene alitoa wito kwa ofisi ya Serikali za mitaa kuwa usafi uliofanyika usiwe tu kutokana na tamko la Mhe. Rais, ila tabia ya usafi ijengeke ndani ya wakazi wa eneo hilo ili kuendeleza usafi wa mazingira katika zahanati na maeneo yote ya wakazi wa Kawe.

Baadhi ya picha mbalimbali za wafanyakazi wa Taasisi ya Mkapa wakiwa kwenye shughuli za usafi katika maeneo ya zahanati ya kawe
Wafanyakazi wa Taasisi ya Mkapa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza kushiriki kufanya usafi katika zahanati ya kawe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...