Serikali imewataka wananchi waliojenga nyumba zao ndani ya soko la Tandale ambalo lipo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam kuzibomoa na kuacha mipaka yote ya soko hilo wazi, na imewapa siku saba kufanya hivyo kabla ya majengo hayo kubomolewa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa George Simbachawene ameyasema hayo tarehe 22 Desemba wakati alipofanya ziara yake katika Manispaa tatu za jiji la Dar es salaam kwa ajili ya kujionea hali ya usafi katika Manispaa hizo.
Akihitimisha ziara yake katika soko la Tandale, Waziri Simbachawene licha ya kuridhishwa na hali ya usafi katika maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam, alisema mipaka yote ya masoko nchini yanapaswa yawe wazi ama sivyo serikali itachukua hatua ya kuyabomoa majengo hayo.
“Wale wote waliotumia njia za ujanja ujanja kuharibu master plan za mipaka ya masoko nyumba zao tutazivunja na tutakutana mahakamani,”alisema.
Alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu ifanyike ili serikali iweze kuruhusu miradi ya maendeleo ifanyike katika maeneo hayo ya masoko na kuongeza kuwa kwa hali ilivyo sasa ni vigumu kwa wafadhili wa miradi kama benki ya dunia kusaidia uimarishaji wa miundombinu ya soko hilo.
Aidha Waziri Simbachawene aliwapongeza wakazi wa jiji la Dar es salaam kwa namna walivyoshiriki katika kufanikisha zoezi la kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao na hivyo kuitikia vyema wito wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Magufuli.
Aliwataka wananchi wote kuuenndeleza utamaduni huu wa kufanya usafi mara kwa mara na kwamba serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa inaandaa mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu wa uzoaji taka katika makazi ya watu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...