Mraghbishi Noorkiyengop Mbaima toka kijiji cha Enguserosambu akisimama mbele ya mifugo iliyokutwa msituni katika eneo lililoruhusiwa la msitu wa jamii wa Enguserosambu

Ilikuwa ni siku ya shangwe na furaha kwa wananchi wa kata ya Enguserosambu wilayani Ngorongoro. Hii ni baada ya serikali kukubali ombi lao la kusimamia rasilimali ya msitu wa Loliondo namba 2 unaopakana na vijiji vinne vinavyokadiriwa kuwa na idadi ya wakazi wapatao 20,000 wanaotegemea mahitaji yao toka katika huo msitu.

Huu ni msitu pekee ambao wananchi kwa kushirikiana na Mkuu wao wa wilaya, na mashirika rafiki, wamefanikiwa kuishawishi serikali kuukabidhi msitu huo kwao. Katika mchakato huo uliochukua miaka kadhaa wanawake toka katika vijiji vya Enguserosambu, Ng’arua, Orkiu na Naan wamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha azma hiyo ya kubakiza msitu wao wa enzi mikononi mwao. Akielezea furaha yake aliposikia msitu wa Loliondo namba 2 umekabidhiwa kwa wananchi, mraghbishi mwanamke Noorkiyengop Mbaima alisema 

“Mimi mwenyewe nimefurahia, kwa sababu sisi akina mama tunategemea sana msitu huu kwa mahitaji yetu. Huu msitu kama ungeondoka katika mikono ya jamii basi tungeathirika sana sisi kina mama.” Umuhimu wa msitu huu kwa kina mama ndio uliowapelekea wao kutunga na kuimba nyimbo za hamasa na kutumbuiza, kushiriki kwa wingi katika vikao mbalimbali vya maamuzi wakati wote wa mchakato huo. 

Kwa kuwa msitu huu ndio tegemeo lao katika kuendesha maisha ya kila siku. Hakuna chochote ambacho kiliamriwa bila ya wao kuchangia na kushirikishwa kuanzia utungaji wa sheria ndogongogo za usimamizi wa msitu hadi kukabidhiwa rasmi msitu huo. “Nikichukulia mfano katika mikutano yote ya vijiji. Kiukweli wanawake wamekuwa wanajitokeza kwa wingi, kuliko makundi mengine yoyote. Hata ile siku ya uzinduzi wa msitu walikuwa wengi zaidi,” anaelezea Jackson Nangiria 

Ushiriki huu wa wanawake unatokana na ukweli kwamba wana uhusiano wa karibu na msitu huo wa enzi wa Enguserosambu.Si kwa ajili yao tu pamoja na watoto wao pia. Ni watoto hawa wa kike wenye majukumu ya kujenga nyumba kwa kutumia miti inayotoka ndani ya msitu huu, ndio wanaotembea na punda wakiwabebesha maguduria ya maji kwa umbali mrefu wakitafuta maji ambayo chanzo chake kipo kwenye msitu huu. Wanapopata watoto wanahitaji dawa za kuwaogeshea na dawa za uzazi ambazo zinatoka kwenye msitu huu. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...