Na Kassim Nyaki.
Watumishi wa Sekretarieti ya Ajira wameaswa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao, kwa kuwa kazi wanayoifanya ni nyeti na inagusa maisha ya watu ambayo itahitaji watu waadilifu, wapenda haki na mfano mwema kwa jamii.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angella Kairuki amesema hayo leo wakati alipotembelea ofisi hiyo na kuzungumza na Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira pamoja na Watumishi.
''Nataka mzingatie uadilifu katika utendaji kazi wenu wa kila siku, maana nitawafatilia kila hatua kwani ninataka Watumishi wa Umma waadilifu ili mwisho wa siku tuwe na Utumishi wa Umma uliotukuka'' alisisitiza Kairuki.
Aliongeza kuwa Watanzania wako wengi wenye sifa za kuajiriwa, ambao wanahitaji kupata huduma bora na inayostahili kwa kuwa kila Mtumishi aliyeko katika Sekretarieti ya Ajira aliajiriwa akijua Utumishi wa Umma una taratibu zake za kiutendaji, kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali na si vinginevyo.
Aidha, aliwataka Watumishi hao kutumia hazina kubwa ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira waliopo kwa kuwa anawafahamu, anajua uwezo wao katika kazi, kwakuwa walikuwa Watumishi  waadilifu wa Umma na wa muda mrefu. Hivyo ushauri wao na maelekezo wanayotoa yakitumika vizuri yataisaidia sana Sekretarieti ya Ajira katika kutimiza malengo yake na kuwa chombo cha mfano wa kuigwa kiutendaji.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Bakari Mahiza alimpongeza Waziri huyo kwa kuchaguliwa kusimamia Wizara hii nyeti inayosimamia rasimaliwatu ambayo ni rasilimali muhimu sana katika taifa lolote na anaamini ujio wake utaongeza chachu katika utendaji wa Taasisi hiyo.

Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Exavier Daudi mbali na kueleza jinsi Mchakato wa Ajira unavyoendeshwa, mafanikio, changamoto na matarajio ya chombo hiko alimshukuru Waziri huyo kwa kuwatembelea na kumwahidi kufanyia kazi maelekezo na ushauri alioutoa.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Daudi Xavier (kulia) akieleza majukumu ya ofisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo. 
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) (kulia) akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki akipata Maelezo ya juu wa upokeaji wa maombi ya kazi kwa njia ya Mtandao kutoka kwa Naibu Katibu wa Kitengo cha TEHAMA Mhandisi Samweli Tanguye.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...