Waziri Mkuu, Kassim Majliwa
akisalimiana na wapigakura wke baada ya kuwasili kijijini kwake Nndagala
wilayni Luangwa kwa mapumziko mafupi Desemba 20, 2015. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………..
*Asema wabadhirifu watang’olewa mara moja
*Asema wako wasomi wengi wanaotafuta ajira
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaonya watendaji wa halmashauri nchini kwamba atakayebainika ametumia
vibaya fedha za Serikali atang’olewa kazini kwa sababu Serikali ya
Awamu ya Tano haina mchezo na mtu.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Desemba 20, 2015)
wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Ilulu uliopo
Lindi mjini.
“Natoa onyo kwa watendaji wote wa halmashauri. Fedha ya Serikali
itakayotumwa kwenu halafu mtu aifanyie ubadhirifu, ole wake. Yeyote
atakayebainika kuzitumia kwa ubadhirifu fedha hizi tutamng’oa. Wako
wasomi wengi huko nje tena wazuri tu, wanasubiri kupata ajira.”
“Nataka watumishi wa umma watambue kwamba Serikali ya Awamu ya
Tano inajielekeza kujali wananchi. Wao wana dhamana ya kuwasilikiliza
na kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanatatua kero zinazowakabili, ”
alisema huku akishangiliwa na wengine wakisema huyu sasa ni Sokoine wa
pili. (Edward Moringe Sokoine alikuwa ni Waziri Mkuu katika Serikali ya
Awamu ya Kwanza).
Waziri Mkuu ambaye amewasili Lindi leo, aliwaeleza wakazi hao
kwamba amekuja kuwashukuru wazee na wana Lindi kwa dua zao na kuwaahidi
kwamba hatawaangusha Rais John Pombe Magufuli na Makamu wake Samia
Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuwatumikia Watanzania
katika ngazi ya Uwaziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia alimpa kazi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Jordan
Rugimbana ya kuhakikisha anaufufua uwanja huo na kuurudisha kwenye enzi
yake ulivyokuwa maarufu katika mikoa yote ya Kusini. “Uwanja huu lazima
uboreshwe kwa sababu unanikumbusha mwaka 1984 wakati nachezea timu ya
Amri Rangers. Kulikuwa na ukoka wa nguvu hapa uwanjani. Kwa hiyo timu
aliyoiunda Mkuu wa Mkoa itafanya kazi lakini pia iwajumuishe Meya na
mbunge wa Lindi Mjini kwa sababu huu uwanja ni mali ya Halmashauri ya
Lindi, ” alisema.
Akielezea kuhusu mipango ya
Serikali kuendeleza sekta ya viwanda, Waziri Mkuu alisema hivi karibuni
mkoa huo utapata wawekezaji kwenye sekta ya gesi baada ya kampuni ya BG
kutoka Uingereza kupata umiliki wa eneo la Kikwetu ili wajenge mitambo
ya kusafisha gesi.
Aliwataka wananchi wa mkoa huo
wawekeze kwenye ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni ili ifikapo
Agosti mwakani, watu wanaokuja kushiriki maonyesho ya NaneNane kitaifa
mkoani humo wasipate taabu ya malazi kama ambavyo imekuwa ikitokea huko
nyuma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...