Na Anitha Jonas –MAELEZO
Wizara ya Nishati na Madini imewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha uzalishaji wa umeme katika Mradi wa Kinyerezi I na Kinyerezi II unakamilika ifikapo mwezi Februari 2016 na kuanza kufanya uzalishaji ilikuongeza kiasi cha nishati ya umeme kufikia zaidi ya Megawati 100.
Agizo hilo lilitolewa leo na Naibu Waziri, Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani alipofanya ziara yake katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya Gesi cha Kinyerezi jijini Dar es Salaam,hii ni baada ya kuelezwa kuwa kituo hicho kwa sasa kinazalisha 70 Megawati za umeme ambaohautoshelezi kwa matumizi ya watanzania.
“Watanzania wamechoshwa na mgao wa umeme na wanaimani kubwa na uzalishaji wa kituo hiki cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi hivyo wanatarajia umeme wa uhakika katika kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji na kujipatia kipato”,alisema Dkt.Kalemani.
Hata hivyo Dkt. Kalemani aliwapongeza watendaji wa TANESCO na wakandarasi wanaosimamia uendeshaji wa mitambo hiyo ya uzalishaji huku akiwasihii waongeze jitihada za dhati kwani watanzania bado hawaridhishwi na kiasi cha umeme kinachozalishwa kwa sasa.
Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omari Chambo alisema kuna mradi mpya uitwao Kinyerezi Extension unakaribia kuanzishwa hivi karibuni ambao utazalisha Megawati 345 za umeme na kupitia mradi huu uzalishaji wa umeme utaongezeka kwa kiasi kubwa.
“Tutajitahidi kwa sasa umeme usikatike mara kwa mara na jitihada za kusafisha mitambo miwili ya phase I na Phase II inafanyika na itakapokamilika tunatarajia kuzalisha zaidi ya Megawati 140 za umeme na usafishaji wake unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu”,alisema Mhandisi Chambo.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Bw.Decklan Mhaiki alisema mradi wa Kinyerezi Extension ambao utagharimu jumla ya kiasi cha Dola Milioni 340 unatarajia kuanza hivi karibuni mara baada ya kukamilika kwa Mkataba na malipo ya 15% kwa mkandarasi.
Pamoja na hayo wizara ya Nishati na Madini imetoa angalizo kwa watendaji wote wanaozalisha umeme kwa kutumia maji walinde vyanzo vya maji na kuacha kutumia maji hayo kwa matumizi mengine kama ya kilimo.
Uzalishaji wa umeme kwa kutumia Nishati ya Gesi utasaidia kupunguza gharama za watumiaji wa umeme pamoja na kushusha gharama za uzalishaji.
Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi
Kalemani (kushoto) akimsikiliza Naibu Mkurugenzi Mtendaji Tanesco Bw.Decklan
Mhaiki alipokuwa akimwonyesha mradi wa Kinyerezi I mara baada ya kuwasili
katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi eneo la Kinyerezi jijini Dar
es Salaam.
Meneja Mradi TANESCO Mhandisi Simon Jalima (wa pili kushoto)
akimwonyesha Naibu Waziri Wizara ya
Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani (wa pili kulia) moja ya mtambo unaopokea
gesi kutoka mtwara na kuisambaza mpaka kituo cha Ubungo alipofanya ziara ya
kuona maendeleo ya mradi huo leo katika eneo la mradi Kinyerezi jijini Dar es
Salaam, wa kwanza kulia ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Tanesco Bw. Decklan Mhaiki.
Meneja Mradi TANESCO Mhandisi Simon Jalima (wa pili kushoto)
akimtembeza Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani (wa
pili kulia) kumwonyesha mitambo mbalimbali ya uzalishaji wa umeme uliyopo
katika kituo hicho cha Kinyerezi I, jijini Dar es Salaam.
: Mmoja
wa wataalamu wa kuendesha mitambo inayosambaza nishati ya umeme uliyozalishwa
kwa kutumia gesi (Shift Supervisor) Bw. Mohamed Lanzi akimwonyesha Naibu Waziri
Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani (wa kwanza kulia) mtambo wa
usambazaji wa umeme wa Morogoro unaotokea Kinyerezi I namna wanavyouendesha.
Meneja Mradi wa
Kinyerezi Extension kutoka Kampuni ya Sumitomo Japan Bw. Shoji Watanabe
akimweleza Naibu Waziri Wizara ya
Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani ni kwa muda gani mradi huo utakamilika
mara baada ya kupewa mkataba wa kuanza kazi hiyo, leo Kinyerezi jijini Dar es
Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...