Serikali imesema ifikapo mwaka 2018 Mfumo wa umeme katika Mkoa wa Kagera utakua umeingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Hayo yalisemwa jana tarehe 27 Desemba na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara mjini Bukoba, Mkoani Kagera ili kukagua miundombinu ya umeme. 
 Ilielezwa kwamba Mkoa huo kwa sasa unapata umeme kutoka nchini Uganda ambao umekuwa ukikatika mara kwa mara na hivyo kulilazimu Shirika la TANESCO kutumia mitambo yake inayotumia mafuta ambayo hata hivyo haikidhi mahitaji ya umeme ya Mkoa. 
 Profesa Muhongo aliliagiza shirika hilo kuhakikisha linaharakisha taratibu za kuunganisha mkoa wa Kagera kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.
"TANESCO ni lazima muharakishe mipango ya kuunganisha mkoa huu kwenye gridi ya taifa ili kuwapatia wananchi huduma ya umeme wa uhakika," aliagiza. 
Aidha, Profesa Muhongo aliiagiza TANESCO kuhakikisha mafuta kwa ajili ya kuendeshea mitambo hiyo yanakuwepo yakutosha kwa muda wote. 
 Alisema ifikapo mwaka 2025, Tanzania itaingia kwenye uchumi wa kati ambao utatokana na uwekezaji mkubwa kwenye viwanda ambavyo vitahitaji umeme wa kutosha na uhakika. 
 Mbali na hilo, Profesa Muhongo aliliagiza Shirika la Tanesco mara baada ya mkataba uliopo wa kuuziana umeme kati ya Tanzania na Uganda kuisha, wahakikishe wanaingia mkataba wa muda mfupi mfupi lengo likiwa ni kuepusha kuwa ndani ya mkataba wakati tayari mkoa huo utakua kwenye gridi ya taifa. 
 Akielezea hali ya umeme mkoani humo, Meneja wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Mhandisi Amos Maganga alisema kwa sasa Tanzania inanunua umeme kwa gharama ya senti za Marekani 8.4 kwa kila unit. Alisema Tanzania inao mkataba wa kununua umeme kutoka Uganda kiasi cha megawati 10 ambao unahudumia wilaya za Bukoba Mjini na Vijijini, Karagwe, Muleba na Misenyi.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto mbele) akimsikiliza  Mhandisi wa kituo cha kufua umeme wa dharura cha Kibeta- Bukoba mjini, Mhandisi Filbert Mlaki wakati wa ziara yake kituoni hapo leo (27 Desemba, 2015). Kituo hicho chenye mitambo minne kinao uwezo wa kuzalisha megawati 2.1 ambacho hutumiwa pale umeme wa kutoka Uganda unapokatika.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella kabla ya kuanza ziara ya kukagua miundombinu ya umeme mkoani humo.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kushoto) akimsikilizaMhandisi Filbert Mlaki.
Waziri wa nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akikagua moja ya mtambo wa kuzalisha umeme wa Kituo cha Kibeta

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...