Mbunge wa Kigoma mjini Mhe. Zitto Kabwe amekabidhi bweni la wanafunzi Shule ya watoto wenye ulemavu wa ngozi Buhangija iliyoko mkoani Shinyanga baada ya kutoa msaada wa kujenga bweni hilo. 
 Katika makabidhiano hayo Mhe.  Zitto alisema Tarehe 18 April mwaka huu alitembelea Shule hiyo akiwa na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Mama Anna E Mghwira kwa lengo la kusalimia watoto na walimu wao na kutazama mazingira ya watoto. 
 "Nilifika hapa kwa lengo la kuona mazingira ya shule na watoto niliona namna Shule ambavyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo haswa nafasi za kulala, Nilishuhudia watoto wakilala karibu watano katika kitanda kimoja. Niliumizwa sana," alisema Zitto kwa masikitiko. Anasema alionyeshwa ujenzi wa Bweni jipya la watoto na kuelezwa kuwa linajengwa na aliyekuwa mrembo wa Tanzania Mwaka 2012, Brigitte Alfred kupitia Taasisi yake ya Brigitte Alfred Foundation. 
 Aidha aliambiwa kuwa ujenzi umesimama kutokana na changamoto mbali mbali ikiwemo ufinyu wa bajeti, "Wakati huo nilikuwa nimeng'atuka Ubunge na nilikuwa nasubiri malipo ya kiinua mgongo Kwa mujibu wa Sheria, niliamua hapo hapo kwamba sehemu ya gratuity yangu nitaitoa kama mchango wangu katika juhudi za Briggitte kuboresha mazingira ya malezi ya watoto wetu katika shule hii." 
 Zitto alisema aliamua pia kusaidia matibabu ya saratani watu wenye ulemavu wa ngozi katika hospitali ya Ocean Road, Dar Es Salaam kupitia fedha hiyo. NaAlisema anamshukuru Mungu kwamba alimuwezesha kutimiza dhamira yake hiyo na hivyo kuchangia juhudi hizi za Briggitte Alfred Foundation kwa Gratuity yake yote ambao sasa umekamilika. 
 "Leo tupo hapa Buhangija kushuhudia ukamilifu wa kazi hii adhimu, nampongeza sana Miss Tanzania 2012 kwa mradi huu unaotoa changamoto kwa watanzania wengine kutumia nafasi zao katika jamii kusaidia jamii yetu," alisema Zitto. 
 Zitto aliitaka Serikali kuhakikisha kuwa Shule muhimu kama Buhangija zinapata uangalizi maalumu kwani mahitaji yake ni maalumu. Alisema nchi yetu haiwezi kuwa na sifa yeyote nzuri duniani kama bado kuna baadhi ya raia wake wanaishi kwa mashaka na hofu ya maisha yao hivyo ni wajibu wa viongozi kuhakikisha kila mtanzania anajivunia badala ya kuvumilia Utanzania wake.
Sehemu ya wanafunzi Shule ya watoto wenye ulemavu wa ngozi Buhangija iliyoko mkoani Shinyanga
Mbunge wa Kigoma mjini Mhe. Zitto Kabwe akiwa meza kuu na mrembo wa Tanzania Mwaka 2012, Brigitte Alfred 
Baadhi ya anafunzi Shule ya watoto wenye ulemavu wa ngozi Buhangija iliyoko mkoani Shinyanga wakiwaimbia wageni wakati wa hafla hiyo
Wageni na sehemu ya wanafunzi Shule ya watoto wenye ulemavu wa ngozi Buhangija iliyoko mkoani Shinyanga

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Safi sana Brigitte Alfred na Zitto Kabwe. Huwa napenda kusikia habari za aina hiyo ambazo zinatia moyo na kuhamasisha. Tuko pamoja.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...