Na Teresia Mhagama, Geita

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani ametoa siku 14 kwa mgodi wa dhahabu wa Buckreef kuanza uzalishaji ama sivyo wataandikiwa hati ya makosa na Afisa Madini Mkazi katika mkoa wa Geita. Naibu Waziri alitoa agizo hilo baada ya kufika katika mgodi huo uliopo katika kata ya Lwamgasa mkoani Geita na kuona hakuna shughuli zozote za uzalishaji zinazoendelea.

“Najua kuwa hamjazalisha dhahabu mpaka sasa, lakini lazima mzalishe ili kulipa kodi na mrabaha, bila kufanya hivyo ndani ya siku 14 zijazo mtaandikiwa hati ya makosa kama sheria ya madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza, mgodi huu mnaumiliki toka mwaka 2011, lazima muanze uzalishaji,” alisema Kalemani.

Aidha Naibu Waziri alisema kuwa mgodi huo umechukua maeneo makubwa ya uchimbaji madini lakini hawayatumii, hivyo wayaainishe maeneo wanayohitaji kutumia na mengine wapewe wachimbaji wadogo.

Akijibu suala la ugawaji wa maeneo kwa wachimbaji wadogo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tanzam2000 inayomiliki mgodi huo kwa ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Joseph Kahama alisema kuwa wako tayari kukaa na Ofisi ya Madini mkoani Geita na STAMICO ili kuainisha maeneo watakayowaachia wachimbaji wadogo.

Kutokana na hilo Naibu Waziri alimwagiza Afisa Madini Mkazi mkoa wa Geita, Mhandisi Laurian Rwebembera kukaa na watendaji wa mgodi huo tarehe 10 mwezi huu ili kuainisha maeneo hayo na kisha wayagawe kwa wachimbaji wadogo.

Awali akizungumza na wachimbaji wadogo katika kijiji cha Lwamgasa, Dkt. Kalemani aliwaeleza kuwa serikali imeongeza kiwago cha utoaji wa ruzuku kutoka Dola za Marekani 50,000 hadi Dola Laki Moja kwa kikundi na kuwaasa wachimbaji hao kujiunga katika vikundi ili kuweza kuwa na sifa ya kupata ruzuku hizo.

“Tunataka ruzuku hizi ziwafaidishe wananchi wengi lakini si mtu mmoja mmoja, ruzuku iwasaidie katika shughuli za uchimbaji madini ikiwemo kununua vifaa vya uchimbaji lakini na ninyi lazima mlipe kodi,” alisema Naibu Waziri.

Awali Mkuu wa mkoa wa Geita, Fatma Mwasa alimweleza Naibu Waziri kuwa maeneo yanayotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ni vyema yakawa yanafanyiwa utafiti ili kuhakikisha kama yana madini na hivyo kuepusha wachimbaji hao kuwekeza katika maeneo yasiyo na madini.

Vilevile alisema kuwa maeneo yanayotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo yagawiwe kwanza kwa wachimbaji wasio na vitalu ili ili kuepusha suala la mtu mmoja kumilikishwa vitalu vingi wakati wengine hawana.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalemani (mwenye suti) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Lwamgasa mkoani Geita wakati alipowatembelea wachimbaji hao ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika shughuli za uchimbaji madini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (mwenye suti) akiwa katika eneo la mgodi wa dhahabu wa Buckreef mkoani Geita wakati alipotembelea mgodi huo na kukuta shughuli za uzalishaji madini zimesimama.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalemani (wa pili kushoto) akizungumza na baadhi ya wananchi katika kijiji cha Lwamgasa mkoani Geita wakati alipofika kijijini hapo ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika sekta za Nishati na Madini.Wa kwanza kushoto ni Afisa Madini Mkazi mkoa wa Geita, Mhandisi Laurian Rwebembera.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalemani (wa tatu kulia) akiwa na watendaji mbalimbali wa kijiji cha Lwamgasa mkoani Geita wakati alipofika kijijini hapo ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika sekta za Nishati na Madini.Wa kwanza kulia ni Afisa Madini Mkazi mkoa wa Geita, Mhandisi Laurian Rwebembera.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...