JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 OFISI YA RAIS

Anuani ya Simu: “TAMISEMI”

Simu Na: (026) 2322848, 2321607

 2322853, 2322420

Nukushi: (026) 2322116, 2322146

2321013 

Barua pepe: ps@poralg.go.tz



Tawala za Mikoa na

Serikali za Mitaa,

S.L.P. 1923,

DODOMA.




TAARIFA KWA UMMA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene (Mb) amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kumsimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa ya Ilala Bw. Dennis. N. Mrema kuanzia leo tarehe 07 Januari, 2016 kwa kosa la kusababisha upotevu wa Mapato ya Serikali kutokana na urasimu wa kukusudia, mazingira ya rushwa na uzembe katika utoaji wa leseni za Biashara.

Kutokana na hali hiyo Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI ameelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kumuondoa kwenye nafasi yake Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa ya Ilala na nafasi yake kukaimiwa na mtu mwingine ili kupisha uchunguzi zaidi juu ya tuhuma zilizotolewa dhidi yake.

Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI amefikia uamuzi huu baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa Wafanyabiashara ambao wamemlalamikia Mtendaji huyu kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za utoaji wa Leseni za Biashara, Urasimu na Mazingira ya rushwa.

Katika uchunguzi wa awali uliofanyika kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Ilala mambo yafuatayo yamegundulika:

(i)                  Ukiukwaji wa Makusudi wa Sheria,  Kanuni  na Taratibu  za utoaji wa Leseni za Biashara.
(ii)               Kutoa Leseni za Biashara zaidi ya 843 bila kuwa na Vyeti vya uthibitisho wa Walipa kodi ‘Tax Clearance Certificates” hivyo kuikosesha Serikali Kodi ya Mapato.
(iii)           Kukaa na fomu za Wafanyabiashara 336 kwa muda mrefu bila sababu za msingi.
(iv)              Kukiuka Mwongozo wa Mkataba wa Huduma kwa wateja ambao unamtaka Afisa Biashara kutoa Leseni za Biashara ndani ya siku 2 hadi 3 baada ya muombaji kuwasilisha maombi yake ya kupatiwa Leseni ya Biashara.

Aidha, Mheshimiwa Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais-TAMISEMI amewaagiza Maafisa Biashara wote nchini watoe huduma za Leseni kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu , kuacha urasimu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Imetolewa na:
   Kitengo cha Mawasiliano  Serikalini
   Ofisi ya Rais-TAMISEMI,



   07 Januari, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Hizi publicity hazina maaana kabisa; Sawa mtu amefukuzwa kazi ila habari hizi kwenye media za nini?? Mbona mataifa mengine watu ufukuzwa kazi bila ya kuhusishwa media au unataka kusema viongozi wa Kitanzania hawawezi kufanya kazi bila ya media????!!

    2: Pili; Ningeomba kabla ya kufukuzisha watu kazi maamuzi yangewahusisha wanasheria wa Serikali ili kuona kisheria ipo sawa kumfukuza mtu kutokana na makosa husika?? Maana hatutaki kuja kupoteza pesa kama fidia kwa fukuza fukuza zinazoendelea nchini; Sheria zifuatwe kikamilifu na maamuzi yote yafuate Sheria na Katiba ya nchi.

    Mwisho; Napenda kutoa pongezi kwa Mh Rais Magufuli kwa uongozi wake imara mpaka sasa na aendelee hivyo hivyo ktk kuliweka Taifa la Tanzania na watu wake ktk mazingira yenye ubora na kulifanya Taifa kuwa imara na nguvu hapa duniani.

    Asante

    ReplyDelete
  2. Kutoa taarifa kwamba mhusika fulani amefukuzwa kazi ni sawa. Lakini kutoa taarifa za mhusika kusimamishwa kazi ili uchunguzi ufanyike inaweza kuwa siyo sahihi. Mara nyingi wahusika wanapokutikana hawana makosa jamii huwa imeshawahukumu na kuwahisi vibaya.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...