[​IMG]

Na. M. M. Mwanakijiji
Mojawapo ya changamoto kubwa zinazoikabili serikali ya Rais J.P. Magufuli inapozidi kujipanga kuleta mabadiliko makubwa ya kimfumo na kifikra katika kuimarisha utendaji wa utumishi wa umma kuelekea 2020 ni watendaji na viongozi ambao bado wanaishi jana wakati nchi iko leo na hivyo wanatishia hatima ya taifa letu kesho.
Jana yetu ni miaka ya nyuma ambapo watendaji waliweza kufanya lolote bila kujali sana matokeo (with impunity) na wafanyakazi walijua watendaji wao walikuwa "hivi na vile" kiasi kwamba watumishi wa chini nao baadhi yao walianza kufanya mambo bila kujali matokeo. Mtu alipopata nafasi ya ajira au kupandishwa cheo fikra za kwanza ambazo inaonekana watu walikuwa nazo ni vipi katika nafasi hizo watachuma kwa haraka haraka kabla mambo hayajabadilika.
Taratibu za ajira na utendaji kazi zilifuatwa kama vile ni jambo la hiari (optional) kiasi kwamba ulazima wa kusimamia sheria na taratibu ulionekana ni usumbufu mkubwa. Mwananchi alipoamua kwenda kupata huduma fulani kwenye taasisi ya serikali ni lazima afikirie mara mbili na kujiandaa kiakili (pyschologically) na usumbufu wowote ambao ataupata. Mwingine inabidi aulize kwanza kama kuna mtu yeyote anayemfahamu huku au kama anafahamu mtu anayeweza kuwa anafahamiana na mtu mwingine huko anakotaka kwenda. Sehemu nyingine katika kutafuta mtu wa kufahamiana naye mtu aliweza kwenda hata kipeo cha tatu na cha nne cha marafiki. Akipatikana anayejuana na fulani huko basi mtu anaweza kua na imani kuwa anaweza angalau kusikilizwa; akikosekana bajeti ya kulainisha mifumo inabidi ifikiriwe tena.
Maisha haya ya jana yamejionesha kwa kiasi kikubwa katika utendaji wa uzembe na usiojali fedha za wnaanchi kama ambavyo ripoti mbalimbali za CAG zimekuwa zikituonesha tangu 2006. Hii jana watu walikuwa wameizoea kiasi kwamba leo haikuruhusiwa ifike kamwe; watu waliipenda jana sana kiasi kwamba hata wakati wa kampeni za uchaguzi bado lilikuwepo kundi la watu ambao waliitamani leo lakini hawakuwa tayari kuiachilia jana.

Matukio karibu matatu yaliyotokea Alhamisi iliyopita yametudokeza kuwa bado tuna tatizo la watu wanaoishi jana. 


Muhimbli ilitarajiwa uongozi mpya kuanza kuondoa kero ambazo si za lazima; hii siyo tu uongozi wa Muhimbili bali pia Wizara ya Afya; lakini inaonekana mazoea magumu. Bado watu wamekutwa tena wamejazana wodini kama vile wako kwenye behewa la Daraja la tatu wakielekea Bara. Hivi kweli bado hakuna mtu mwenye akili za 'kawaida' tu kuwa watu wanaohitaji huduma safi, salama na mazingira mazuri kabisa ya tiba ni kina mama na watoto - kwa sababu ya udhaifu (vulnerability) yao? Kama watu hawa wanashindwa kuliweka hili kama ajenda yao nambari 1 hivi huko kwingine watapanga nini? Kama inabidi kufuta posho na mishahara ya viongozi wote ili kina mama na watoto wetu wapatiwe huduma sahihi na bora basi na liwe hivyo; lakini hili halieleweki?

Kabla hatujatulia Mhe. Mwigulu Nchemba naye kazukia huko Pugu (kwa mara nyingine) kufuatilia machinjio. Akakuta kati ya ng'ombe 200 waliokuwa wanaenda kuchinjwa (au sijui wameshachinjwa) ni 20 ambao walikuwa na vibali; huku wale wengine wote kama wamelipiwa basi wamelipiwa kwenye mifuko ya mtu na labda kwa kiasi cha chini kidogo na hivyo kuikosesha serikali mapato; na hilo ni siku moja tu! Hawa watu wa machinjioni walikuwa wanaamini basi ile ya kwanza ni nguvu ya soda basi wacha waendelee kama ilivyokuwa (status quo was maintained). Hawakuwa tayari kuamini kuwa mtu atarudi tena na inawezekana hata watakaoingia bado watafikiria Mwigulu hatawazukia tena na hivyo wataanza na wao kutafuta 'mitkasi' ya hapa na pale. Warudi jana.

Na kabla hata hatujatulia Waziri Mkuu Kassim "Tabasamu" Majaliwa (nimempa jina la 'tasabamu' kwa sababu tabasamu lake linadanganya watu) karudi tena Bandari ambako nako akakuta madudu mengine yale yale na tena safari hii ikitisha zaidi. Kwamba, mpango wake wa kwenda huko kwa kushtukizwa baada ya kutoshwa na watumishi safi ukatibuliwa na 'mmbeya' mmoja kiongozi wa juu tu ambaye aliamua kuwadokeza na hivyo kutaka kusaidia kuficha madudu huko.
Nakubaliana na wengine wote kuwa Kiongozi  huyo akithibitika kweli ametuma ujumbe wa kumtonya mama Chuwa ili ajaribu kuvuruga ushahidi basi Magufuli hana jinsi; ni lazima amuondoe bila kujali uwezo wake, ujiko wake, au sifa zake. Serikali hii haipaswi na haitakiwi hata kuuliza "mwenzetu ilikuwaje ukavuruga mipango ya waziri Mkuu". Hii ni hujuma ya ndani (internal sabotage). Tena hili inapaswa lifanyiwe kazi mapema sana ili kuleta heshima na woga kwa viongozi wengine. Magufuli akipepesa macho tu na kujikwaa tu atajitengenezea udhaifu usio wa lazima.

Nina uhakika wapo viongozi wengine na watumishi wengine ambao bado na wenyewe wanaombea kuwa safishasafisha hii haitowafikia na kwamba, hizi zote zilikuwa nguvu za soda. Siku 100 baadaye nguvu za soda bado zinachemka na kama tulisikia dokezo kidogo Bandari ni moja tu ambako kunahitaji kusafishwa ili safisha hii iendelee maeneo mengine. Hawa wa sehemu nyingine kama wana akili timamu wanapaswa ama kuanza kujiondoa wenyewe au wasubiri shoka la Magufuli liwekwe kwenye mashina yao!
Jana imepita; waliotumikia fikra za wa jana wajue kuwa siku mpya imefika. Hili nililisema mwanzoni lakini bado watu hawaamini kuwa kuna siku mpya. Hawaamini kuwa kiongozi huyu siyo yule na fikra zinazomuongoza siyo zile. Waliozoea kubebana, kufichiana na kusaidiana kufika hujuma, rushwa, magendo na hujuma za kila namna wakati wao uliishia jana.

Ni lazima washughulikiwe leo kama tunataka kesho iliyo bora; kama tunataka watoto wetu na vijana wetu wanafikiria kutumikia umma kuwa na misingi mizuri, ni lazima uchafu wa jana usafishwe. Usafishwe na kila mtu ajue kuwa tunahitaji utumishi wa umma ulio msafi na ambao uchafu kidogo tu ukitokea hauchelewi kushughulikiwa. Na katika kushughulikia ni lazima tuwatoe mfano wale wenzetu wote ambao tulidhani wanaijua leo lakini bado kifikra wametiwa pingu za jana na bado hawajaziachilia; kwani hawa ni hatari kwa kesho yetu na ya keshokutwa ya watoto wetu na mtondogoo wa watoto wa watoto wetu.
Siku mia zimepita lakini siku mamia bado zinakuja. Mwendo wa kurudisha heshima katika utumishi wa umma na weledi wa watumishi unapaswa kuongeza kasi. Mpaka Watanzania tuheshimiane na tuheshimu utumishi wa umma.
Hadi hivi sasa hakuna majuto.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. The mdudu, Asante sana ndugu M M Mwana kijiji fikla zako na za kwangu ziko pacha ila mm tatizo langu kwenye kuandika kama ww ndugu zangu watanzania hizi changamoto zilizo chambuliwa hapo juu ni ukweli mtupu pasipo kumung'uunya maneno hongera sana M M Mwana kijiji so watumishi wote wa uma ndugu zangu lazima mbadilike na muachane na mambo ya kijinga ya umungu watu, rushwa, ufisadi, kufanya kazi kwa mazoea pasipo na ubunifu, pasipo na uzalendo, uzembe wa kijinga na mwisho kabisa ondokaneni na gonjwa la Uccm na Ukawa na msikubali kutumiwa na wana siasa watakutoweni#kafaraaa amkeni usingizini hii ni serikali ya awamu ya 5 chini ya Rais Magufuli na team yake so hakuna kulala na msipo badilika nyie watumishi wa uma basi tuta kupokeeni mitaani mmoja baada ya mwingine na tuta kuchekeni kwa kejeri na dharau la sivyo mpige kazi kweli kweli kama watumishi wa uma

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...