Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali juu ya kitendo cha kushambuliwa na kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa kike wa Kitanzania nchini India. 
Hatua hizo ni pamoja na kikao chake na Balozi wa India hapa nchini, Mhe. Sandeep Arya ambapo Serikali ilimtaka Balozi huyo kufikisha ujumbe nchini kwake wa kuwahakikishia ulinzi raia wa Tanzania waliopo India na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo. Mkutano ulifanyika Wizarani tarehe 04 Februari, 2016.

Sehemu ya Waandishi wa Habari waliohudhuria Mkutano huo. 
Mkutano ukiendelea.

Serikali ya Tanzania imesikitishwa na inalaani vikali kitendo cha udhalilishwaji alichofanyiwa mwanafunzi wa kike wa Kitanzania na Kundi la watu katika jimbo la Bangalore nchini India.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi alipokutana na Wandishi wa Habari kwa ajili ya kuwaeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia kitendo hicho cha kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa Kitanzania nchini India.
Balozi Mwinyi alisema kuwa, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na Ubalozi wa Tanzania nchini India kuiandikia Serikali ya nchi hiyo kuomba maelezo kamili kuhusu tukio hilo pamoja na kuitaka Serikali ya India kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika pamoja na kuimarisha usalama katika maeneo wanayoishi wanafunzi wa Kitanzania. 
Aidha, Balozi Mwinyi alieleza kuwa amemwita Balozi wa India hapa nchini, Mhe. Sandeep Arya na kumweleza masikitiko ya Serikali ya Tanzania kufuatia kitendo hicho cha kushambuliwa na kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa kike kutoka Tanzania.
Katika mazungumzo yao, Balozi Arya alieleza bayana kuwa Serikali ya India imesikitishwa na tukio hilo la udhalilishaji na kwamba Serikali imeahidi kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kutekeleza uovu huo.
Alisema kuwa Waziri Mkuu wa Jimbo la Bangalore aliongea na umma kuelezea masikitiko yake kuhusu uovu huo na kuahidi kuwa mamlaka za jimbo hilo zitaimarisha usalama katika maeneo yote wanayoishi wanafunzi wa Tanzania na raia wengine kutoka nje.
Balozi Arya aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa India inaheshimu ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na nchi yake, hivyo itashughulikia suala hilo kwa ukamilifu na hadi wakati huu tayari watu watano wanashikiliwa na vyombo vya usalama wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo. 

Sanjari na taarifa hiyo, Balozi Mwinyi aliwaomba Watanzania kutohusisha tukio hili la uhalifu na ajali ya Mtanzania, Bw. Christian Benjamin Mlyansi iliyotokea nchini India jana usiku na kusababisha kifo chake. Alisema kuwa Bw. Mlyansi alipata ajali ya kawaida alipokuwa anaendesha pikipiki ambapo ilipoteza mwelekeo na kugonga ukingo wa kati wa barabara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. HIYO KULAANI TU HAITOSHI, WAZIRI MKUU WA JIMBO LA KARNATEKA HUKO INDIA ALISEMA KUWA HUYO "MSICHANA MTANZANIA ASINGEDHALILISHWA KAMA HUYO MWAFRIKA MSUDANI ASINGEMGONGA NA KUMUUA MUHINDI HUYO" HAYO NI MANENO YA KIBAGUZI NA YASIYO NA HEKIMA HATA KIDOGO!! JE MTU MWINGINE AKIFANYA KOSA MWINGINE WA RANGI INAYOFANANA ATAKUWA NA KOSA? KWA NINI WATU NA SERIKALI YAKE ITOE "COLLECTIVE PUNISHMENT" KWA HUYO MWANAFUNZI NA WENZAKE WASIYEKUWA NA HATIA?? SERIKALI YETU INAKOSEA SANA....HILO TATIZO LA KUONEWA KWA WATU WA RANGI NYINGINE NA LA RACE (CASTE SYSTEM) NI LA KAWAIDA KWA WAGENI WOTE HALAFU LEO TUNAFIKIRIA KUWASAPOTI INDIA ILI IWE MJUMBE WA KUDUMU KWENYE UNITED NATIONS? ANATAKIWA WAZIRI MAHIGA ASIMAME KWENYE PODIUM ATOE MSIMAMO WA TANZANIA NA JINSI AMBAVYO WATANZANIA WAMECHUKIZWA NA LILILOTOKEA NA AELEZE JINSI GANI AMBAVYO RAIA WA INDIA,WAGENI KUTOKA INDIA NA WAHINDI RAIA WANAVYOISHI KWA AMANI KATIKA NCHI YETU WANAVYOISHI KWA AMANI BILA KUBAGULIWA. KUTOA "VERBALE NOTE" PEKEE KWA SERIKALI YA INDIA BADO HAITOSHI NA SIDHANI KAMA HILO NI SULUHISHO KWA SABABU HAYA MATATIZO YANAJIRUDIA RUDIA KILA MARA HUKO INDIA NA MAPOLISI WALIOKUWEPO BADALA YA KUMUOKOA HUYO MSICHANA MTANZANIA WAO WALIKUWA WAANGALIAJI TU KITU AMBACHO KINAONYESHA WALIKUWA WAKIPENDEZWA NA KILICHOKUWA KIKITOKEA.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...