Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), linapenda kuchukua fursa hii kukanusha taarifa iiliyochapishwa kwenye Gazeti la Mtanzania la Jumapili tarehe 7 Februari 2016 Toleo Na: 8087 lenye kichwa cha habari ‘TPDC kwafukuta’.  Taarifa hii si sahihi na ina lengo la kulichafua Shirika na kuupotosha umma wa Watanzania.

TPDC ni Shirika la Umma, linalomilikiwa kwa asilimia mia moja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo taratibu za kuliendesha Shirika hufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi. 

Hii ina maana kwamba, taratibu za kupata Kampuni ya kufanya Utafiti wa Vitalu vya mafuta na gesi kwa kutumia teknolojia ya ‘Airborne Gravity Gradiometry’   ilifuata sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 pamoja na kanuni za manunuzi ya umma za mwaka 2013. 

Aidha, tungependa kuwafahamisha watanzania kwamba taarifa iliyotolewa na gazeti la Mtanzania zilikuwa zina lengo la kupotosha umma kwani zoezi zima la kutafuta mkandarisi lilikuwa la wazi na lilihusisha kampuni tatu ambazo ni Bell Geospace ya Marekani, CGG ya Ufaransa na ARKEX ya Uingereza ambazo ndizo kampuni pekee zenye uwezo wa kutumia teknolojia tajwa hapo juu. 

Kutokana na kuwepo kwa kampuni tatu tu hapa dunia zenye utaalamu uliohitajika, Shirika liliwasiliana na kampuni husika kwa mujibu wa kanuni ya manunuzi  ya umma ya mwaka 2013 namba 152(1) (b) ili kuwasilisha taarifa za kiufundi na kifedha  kwa TPDC.

Baada ya taratibu hizo za manunuzi kufanyika, ndipo kutokana na tathimini iliyofanyika, Kampuni ya CGG ndiyo iliyopewa kazi ya kufanya utafiti maeneo yafutayo; Eyasi – Wembere iliyopo Manyara, na Mandawa Mkoani Lindi wakati Lake Tanganyika North iliyopo Kigoma, ilifanywa na kampuni ya Bell Geospace. 

“Airbone Gravity Gradiometry” ina gharama nafuu, inachukua eneo kubwa la utafutaji na kwa kipindi kifupi sana. Ni aina ya teknolojia inayotafiti maeneo mapya ya utafutaji na yale ambayo tayari yameshaonyesha dalili nzuri za utafutaji wa hapo awali. Imechukua miezi mitatu tu kwenye maeneo tajwa hapa nchini kukamilisha kazi ya kukusanya data.

TPDC inakanusha vikali kuwepo kwa shinikizo toka kwa Mtu au Taasisi yoyote katika kufanikisha zoezi hili, aidha Shirika linasisitiza kuzingatiwa kwa utaratibu wa sheria za manunuzi na hivyo kuwataka Watanzania kupuuza taarifa hizi zilizotolewa na gazeti la Mtanzania kwani ni za uzushi na upotoshaji mkubwa.

Tunawaomba wadau wote wa sekta ndogo ya mafuta kuendelea kufanya kazi za utafiti, utafutaji na uendelezaji wa sekta nzima ya gesi asilia.

“Gesi Asilia kwa Maendeleo ya Taifa”

Imetolewa na:
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji
Shirika la Maendeleo ya Petroli ya Tanzania

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...