Aliyekuwa Mhasibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani katika jeshi la kuzima moto na uokozi na Bw. Naamini Hendry Sangiwa pamoja na
Mkandarasi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiareni Investment Ltd Bw. Webu Manoth Masawe wamehukumiwa leo
tarehe 24/3/2016 kwa kesi ya kuhujumu uchumi katika Mahakama ya wilaya ya
Ilala. Hukumu hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Hassan.
Washtakiwa tajwa hapo
juu walishtakiwa kwa makosa 7 yakiwemo Matumizi Mabaya ya Madaraka, Kutumia
Nyaraka Kumdanganya Mwajiri kinyume na kifungu cha 22 na 31 mtawalia vya Sheria
ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007, Kughushi Nyaraka kinyume na
Kifungu cha 333, 335 (d) (1) na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16,
na kuisababishia Serikali hasara kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza,
Kifungu cha 57(1) na 60(1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200.
Mnamo mwaka 2009
Serikali ilitoa zabuni ya Ujenzi wa uzio wa Chuo cha Zimamoto na Uokozi
kilichopo Mbopo Bunju katika Manispaa ya
Kinondoni Jijini Dar es Salaam. Kampuni ya Kiareni
Investment Ltd (Mzabuni), ilipatiwa zabuni hiyo na kulipwa Kiasi cha Shilingi 81, 963, 360/=. Hata hivyo
taratibu za utoaji zabuni hazikufuatwa, na Mzabuni ambaye ni Kampuni ya Kiareni
Investment Ltd, alifanya kazi yenye thamani ya kiasi cha Shilingi 13, 784, 652/= tu kati ya fedha yote aliyolipwa. Ili
kuwezesha malipo ya Shilingi 81, 963,
360/= kulipwa pasipo kazi kukamilika, Washtakiwa walitoa zabuni kwa
Mkandarasi pasipo Mkataba (LPO), na
Kughushi Hati ya kuonesha kazi imekamilika (Certificate
of Works Completion).
Washitakiwa wote watatu walifikishwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Ilala mwanzoni mwa mwaka 2014 na kusomewa mashtaka yao
Mbele ya Hakimu Mkazi Hassan, ambapo washitakiwa walifunguliwa kesi ya Uhujumu
Uchumi No. 06/2014. Upande wa Jamhuri katika Kesi hii uliwakilishwa na Wakili STANLEY HILMAR LUOGA akisaidiana na
Wakili EMMANUEL
JACOB,
wote waendesha Mashitaka wa TAKUKURU Makao Makuu. Upande wa washtakiwa wote
waliwakilishwa na Wakili wa Kujitegemea MDUMA.
Upande wa Jamhuri uliita Mashahidi 7 na kupeleka vielelezo 21 ili kuthibitisha
kesi dhidi ya washtakiwa. Upande wa washtakiwa hawakuita shahidi hata mmoja
walijitetea wenyewe.
Mshitakiwa wa kwanza Dotto Salehe Mgogo, ambaye alikuwa
Kaimu Mkuu wa Mafunzo wa Wizara ya Mambo ya Ndani katika idara ya Jeshi la
Zimamoto na Uokozi alifariki dunia mwaka 2014 baada ya kusomewa mashitaka na
hivyo Mashitaka dhidi yake yalifutwa kwa mujibu wa sheria. Kufuatia kifo cha
Mshitakiwa wa kwanza,
Mshitakiwa wa Pili Bw. Naamini Hendry Sangiwa ambaye
alikuwa Mhasibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Katika Jeshi la Zimamoto na
Uokozi alikuwa anakabiliwa na makosa manne (4) ambapo makosa mawili ni ya
Matumizi Mabaya ya Madaraka, Kughushi na Kuisababishia Serikali Hasara, ametiwa
hatiani katika makosa yote mawili ya Matumizi ya Madaraka na kupewa adhabu ya
kulipa faini ya Tshs.300, 000 kwa kila kosa la Matumizi Mabaya ya Madaraka kama
atashindwa kulipa faini, kwenda jela miezi 6 kwa kila kosa. Katika Kosa la
Kughushi Nyaraka, Mshtakiwa ametiwa Hatiani na Kuamriwa kutotenda kosa lolote
la jinai kwa muda wa miezi 12.
Mshitakiwa wa tatu
ambaye ni Bw. Webu Manoth Masawe,
ambaye ni Mkandarasi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiareni Investment Ltd,
anakabiliwa na Kosa moja la Kuisababishia Serikali Hasara. Mahakama imemtia hatiani na kumpa adhabu ya kwenda
Jela miaka mitatu (3) pamoja na Kuirudishia Serikali kiasi cha Shilingi 67,
913, 748/= ikiwa ni hasara aliyoisababishia Serikali.
IMETOLEWA
NA OFISI YA AFISA UHUSIANO
TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA
24 MACHI, 2016
The mdudu, safi sana hii ndio serikali ya awamu ya 5 hakuna kucheza na Mafisadi, Wezi, Wazembe, Wavivu na wahujumu uchumi wote funga lupango new Tanzania is coming soon
ReplyDelete