Na Nuru Mwasampeta
Imeelezwa kuwa mgogoro baina ya wachimbaji wadogo wa madini katika eneo la Uwaseke wilayani Iramba mkoa wa Singida na kampuni ya Meek Mines umemalizika baada ya Serikali kutoa ahadi ya kutoa ufumbuzi ndani ya siku Saba.
Hayo yamebainika mwishoni mwa wiki baada ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Merdard Kalemani kufanya ziara katika eneo hilo lenye mgogoro na kusikiliza malalamiko ya pande zote zinazohusika katika mgogoro huo.
Ilibainishwa kuwa wachimbaji wadogo wa eneo la Uwaseke mkoani humo waliingia ubia na kampuni ya Meek Mines kwa makubaliano ya kampuni husika kutoa ajira kwa wachimbaji wadogo wa eneo hilo lakini makubaliano hayo hayajafanyiwa kazi kwa kipindi cha miaka minne sasa na kuwafanya wakazi wa eneo husika kukosa kipato.
Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali itatoa tamko rasmi ndani ya siku Saba litakalowezesha shughuli za uchimbaji kuendelea na hivyo kuchangia pato la taifa kupitia kodi mbalimbali na mrabaha unaolipwa serikalini.
“Suala la eneo hili kutofanya uzalishaji kwa kipindi kirefu kumeipotezea Serikali mapato mengi sana hivyo ni lazima suala hili tulitatue haraka iwezekanavyo,” alisema Dkt. Kalemani.
Kwa upande wake Kamishna wa Madini kanda ya Kati, Sostheness Massola alisema kuwa amefarijika sana kwa ziara hiyo ya Naibu Waziri ambayo imetoa muongozo wa utatuzi wa mgogoro huo.
“Naibu Waziri tunashukuru sana kwa kufika katika eneo hili kwani mgogoro huu umekuwa wa kipindi kirefu lakini sasa ufumbuzi utapatikana kwani umeshatoa maagizo yatakayotatua mgogoro huo,” alisema Massola.
Makubaliano kati ya kampuni ya Meek Mines na Uwaseke yalifanyika mwaka 2012 na sasa wananchi wanaomba mkataba huo kusitishwa ili waendelee na shughuli zao bila kuihusisha kampuni hiyo kama ilivyokuwa awali.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...