Na Veronica Simba
Serikali ya Tanzania imeendelea kupokea maombi ya wawekezaji hususani
katika miradi mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji umeme.
Hivi karibuni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
alikutana na kuzungumza na Ujumbe kutoka Kampuni ya NARI Group
Corporation ambayo ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Gridi ya Taifa la
China, ambao walimweleza Waziri kuwa, pamoja na madhumuni mengine,
wana nia ya kuzalisha umeme.
Makamu Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Bao Tianhua alimweleza Waziri
Muhongo kuwa, Kampuni yake inao mtaji wa kutosha pamoja na teknolojia
ya kisasa katika uzalishaji umeme. Aliongeza kuwa Kampuni ya NARI ina
uzoefu mkubwa katika kutekeleza miradi ya umeme kwani ilianza kufanya
kazi kutoka miaka ya 1960.
Akijibu swali la Waziri kuhusu kiwango cha umeme ambacho Kampuni
yake imejipanga kuzalisha endapo itakubaliwa maombi yake, Tianhua
alisema wamejipanga kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 300 hadi
400 kwa kuanzia.
Akieleza zaidi kuhusu nia ya Kampuni yake kuwekeza katika uzalishaji wa
umeme nchini, Tianhua alisema kuwa wangependa kushirikiana na Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco) katika mradi huo ambapo NARI
watawezesha masuala yote ya kiuchumi katika mradi.
Vilevile, alisema kuwa lengo lao ni kuzalisha umeme kwa kutumia gesi
kupitia teknolojia ijulikanayo kitaalam kama ‘combined cycle’.
Akitoa mwongozo kuhusu maombi yaliyowasilishwa, Profesa Muhongo
aliwataka wawekezaji hao kukutana na kuzungumza na TANESCO pamoja
na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ili kujadili kwa kina
kuhusu mapendekezo husika na kwamba, iwapo maombi yao
yatakubaliwa, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja (Aprili 15 mwaka huu),
NARI wanatakiwa wawe wamethibitisha iwapo watafanya uwekezaji huo
ama la.
“Muda tunaotoa kwa sasa si zaidi ya mwezi mmoja, hivyo ndani ya mwezi
mmoja, iwapo maombi yenu yatakuwa yamekubaliwa, mtapaswa kuwa
mmewasilisha jibu lenu.”
Aidha, Waziri Muhongo aliwataka NARI kuwasilisha kwa TANESCO na
EWURA mapendekezo mengine waliyowasilisha kwake kuhusu nia ya
kuwekeza katika miradi ya umeme vijijini kwa kutumia teknolojia ya
makontena maalumu pamoja na miradi ya umeme jua. Aliwataka
kuzungumzia hayo katika kikao kilichopangwa kufanyika baina yao.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto),
akimsikiliza Meneja wa Kanda ya Ulaya na Afrika wa Kampuni ya NARI
Group, Chen Chao wakati alipokutana na Ujumbe kutoka Kampuni hiyo hivi
karibuni Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Waziri
ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia
masuala ya Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo pamoja na Viongozi
na Maofisa waandamizi wa Wizara. NARI wameonyesha nia kuwekeza
katika uzalishaji umeme.
Makamu Meneja Mkuu wa Kampuni ya NARI Group, Bao Tianhua
(Kushoto), akimkabidhi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo (Kulia) zawadi ya picha ya mmoja wa miji maarufu ya China.
Anayeshuhudia ni Meneja wa Kampuni hiyo kwa Kanda za Ulaya na Afrika,
Chen Chao. Ujumbe kutoka Kampuni ya NARI Group ulikutana na Waziri
Muhongo hivi karibuni Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam na
kuonyesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa umeme.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia
masuala ya Nishati, Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo ( wa pili – kushoto),
akizungumza jambo na Meneja wa Kampuni ya NARI Group kutoka China,
Chen Chao (Kulia) mara baada ya kikao baina yao na Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambapo walionesha nia ya kuwekeza
katika uzalishaji wa umeme.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...