Na Lorietha
Laurence-Maelezo
Jamii nchini imeaswa kuendelea kujenga familia imara kwa kuwa ndicho
kitovu cha mabadiliko katika jamii na maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, imekumbushwa kuwa masuala
mbalimbali hujadiliwa, kupangwa na
kutekelezwa kuanzia ngazi ya familia kwa ajili ya kuimarisha ushiriki thabiti
wa jamii katika maendeleo ya taifa.
Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii
,Jinsia, Wazee na Watoto wakati wa maadhimisho ya Siku ya familia iliyofanyika Mei, 15, 2016.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Tanzania iliadhimisha siku hiyo chini ya kauli
mbiu ya isemayo “Familia Yenye Afya Bora ni Mwanga wa Maendeleo”
Taarifa hiyo imebainisha kuwa familia
ni kitovu cha Maendeleo katika jamii hivyo haina budi kutambua kuwa uzingatiaji
wa masuala ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi hupaswa kujadiliwa, kupangwa na
kutekelezwa kuanzia ngazi ya familia kwa ajili ya kuimarisha ushiriki thabiti
wa jamii katika maendeleo ya taifa.
Imebainisha
kuwa maendeleo ya nchi hayawezi kufikiwa kama familia hazitakuwa na afya
bora hivyo kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuchochea mafanikio ya malengo ya
Maendeleo Endelevu yatakayozingatia uboreshaji wa huduma ya afya bora ya
familia, malezi bora ya watoto na utunzaji wa afya ya watu wenye mahitaji
maalum wakiwemo wazee na watu wenye ulemavu.
“ Kila
mwanafamilia anahitajika kushiriki katika maadhimisho ya siku hii muhimu kwa
kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo, ikiwemo vyombo vya habari kuelimisha wananchi kuhusu
umuhimu wa maadhimisho haya ili kuharakisha uboreshaji wa afya za wanafamilia
wote katika nchi yetu” imeeleza sehemu taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao
wa Jinsia Nchini (TGNP) Bi. Lilian Liundi akiizungumzia siku hiyo katika mahojiano
maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) ameeleza kuwa hali ya familia
katika maeneo mbalimbali haiko salama kutokana na changamoto za kiuchumi.
Ameeleza
kuwa kumekuwa na changamoto ya tatizo la mimba za utotoni kwa watoto wa kike na
wanawake kuachiwa familia hivyo misingi ya familia inakuwa siyo bora kutokana
na kuwepo kwa malezi ya upande mmoja.
Naye
mchambuzi wa Masuala ya Siasa kutoka nchini Kenya Bw. Bobby Mkangi ameeleza kuwa kufuatia hali ngumu ya uchumi
misingi ya familia imevurugika na hivyo kupelekea kuwepo na ajira za watoto
ambao badala ya kuwa shule wanafanya kazi ndogondogo kusaidia kipato cha
familia.
Siku ya Familia Duniani huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa kwa mujibu wa Tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa namba 47/257 la
Septemba 20, 1993.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...