Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya
MINJINGU Mines & Fertliser Ltd ya Arusha wametia sahihi Hati ya
Makubaliano (MoU) kushirikiana katika kufanya tathimini za kina
katika kitalu cha Songo Songo Magharibi.
Akiongea baada ya kutia sahihi hati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa
TPDC, Dkt. James Mataragio alisema makubaliano kati ya TPDC na
Kampuni ya Minjingu yanafungua fursa ya kufanya tathmini za
kitaalamu kwa pamoja juu ya takwimu zilizopo za kitalu cha Songo
Songo Magharibi ambacho kinamilikiwa na TPDC nia ikiwa ni
kutafuta mashapo ambayo yanaweza kuhifadhi mafuta au gesi
asilia.
“TPDC tayari ina takwimu nyingi kuhusu Kitalu cha Songo Songo
Magharibi na itafanya kazi kwa karibu na Kampuni ya MINJINGU
kuhakikisha kunakua na mafanikio katika mradi huu” amesema Dkt
Mataragio.
Dkt. Mataragio amesisistiza kuwa makubaliano hayo yanatoa
wajibu kwa pande zote mbili kufanya kazi kwa pamoja ndani ya
kipindi cha mwaka mmoja kutathmini uwezekano wa mashapo ya
kitalu cha Songo Songo Magharibi kuhifadhi mafuta au gesi.
“Iwapo kutakua na matokeo chanya basi hatua zingine za utafiti
ikiwemo kuchimba kisima zitafuata” aliongezea Dkt. Mataragio.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Minjingu, Ndugu Pardeep Hans
alisema wao kama kampuni ya kizawa wamefurahi sana
kuaminiwa na Serikali na watafanya kazi kwa weledi wa hali ya juu
wa kushirikiana na TPDC ili kuhakikisha wanafikia lengo la
ushirikiano wao.
“Endapo gesi itagundulika basi itatumika kutumika katika mradi wa
mbolea ambao MINJINGU wako ubia na TPDC” pamoja na
Ferrostaal kutoka Ujerumani, Haldor Topsoe ya Denmark na Fauji
ya Pakistani” alisema Bw. Hans.
Makubaliano hayo ya awalia yanafungua fursa ya TPDC pamoja na
MINJINGU ya ushirikiano wa utafiti katika Kitalu cha Songo Songo
Magharibi, Kampuni ya Mijingu ikiwa Kampuni ya kwanza ya
Kizawa kushirikiaa na TPDC katika utafiti wa mafuta na gesi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio (kushoto) na
Mkurugenzi wa Minjingu, Bw. Pardeep Hans wakipeana mikono mara
baada ya kutiliana sahihi Mkataba wa Makubaliano (MoU) katika
utafiti wa mafuta na gesi na kufanya tathimini za kina katika Kitalu
cha Songo Songo Magharibi.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...