WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
WIZARA
YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KULAANI MAUAJI YA WATU
SABA (7) WA FAMILIA MOJA WILAYANI SENGEREMA MKOA WA MWANZA
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na watoto imesikitishwa na tukio la mauaji ya watu saba wa familia moja
waliokatwakatwa mapanga baada ya kuvamiwa nyumbani, katika kijiji cha Sima
wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, siku ya Jumatano usiku.
Wizara inalaani vikali mazingira ya mauaji ya
watu hao wa familia moja, ambapo wauaji walivamia nyumba ya mama mjane na
kumuuwa yeye mwenyewe, na watu wengine sita wakiwemo watoto watatu.
Wizara inapongeza utayari
wa uongozi wa mkoa wa Mwanza na jeshi la Polisi amabo waliweza kufika sehemu ya
tukio ili kufuatilia mauaji hayo. Ni imani ya Wizara kuwa Polisi kwa
ushirikiano wa wananchi wa wilaya ya Sengerama wataweza kuwasaka watuhumiwa wa mauaji
na kuwachukulia hatua kali.
Wizara inawasisitiza
wananchi kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuwamata watuhumiwa ili kuondoa hofu
miongoni mwa familia za kijiji cha Sima na wilaya ya Sengerema. Kukamatwa kwa watuhumiwa
hao kutarejesha imani na utulivu miongoni mwa wakazi wa Sengerema na hivyo kuweza
kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Wizara inasisitiza
kwamba kila binadamu anayo haki ya kuishi na
kupata hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa Sheria za nchi. Vitendo vya mauaji ya kikatili vinapotokea katika familia zetu
vinasababisha hofu kubwa miongoni mwa wanafamilia. Mauaji hayo yanawakosesha
amani wanafamilia na yanadhohofisha ari ya ndugu wa familia kufanya shughuli zao
kwa amani.
Wizara inaomba
wanafamilia waliopoteza ndugu zao kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki
cha majonzi makubwa, wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kuwasaka
watuhumiwa wa mauaji hayo.
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto. 12/5/2016
Poleni wafiwa. Kila mtu athamini uhai mauaji ya kiholela yasipate nafasi.
ReplyDelete