Baada ya kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa , timu ya soka ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imebakiza mitihani miwili kabla ya kuandika historia ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, imefahamika.

Mtihani wa kwanza ni mchezo dhidi ya Afrika Kusini unaotarajiwa kufanyika ama Agosti 5, 6 au 7, 2016 ambako mechi ya kwanza itapigwa ugenini kabla ya kurudiana jijini Dar es Salaam, Tanzania wiki moja baada ya mchezo huo. Hivyo mchezo wa marudiano utafanyika Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamzi Agosti 14, 2016 saa 9.00 alasiri.
Mshindi wa jumla katika michezo hiyo, itacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville. Wakati Afrika Kusini imepitishwa moja kwa moja Namibia imepenya kwa kuiondoa Botswana licha ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wake uliofanyika jana Julai 2, 2016 huko Botswana.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Namibia, Juni 24, mwaka huu wenyeji (Namibia) walishinda 1-0. Kwa msingi huo, Namibia imepenya kwa bao la ugenini ililolivuna katika mchezo wa jana. Bao la ugenini imefanya kuwa na mabao 3-2.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Nyundo Shime, ameangalia ratiba ya mlolongo huo na kusema “Ushindani utakuwa mkubwa, lakini mimi nimelenga kushinda michezo yote iliyo mbele yangu. Si kwamba napigania kufuzu kwenda Madagascar tu kwenye fainali za Afrika, la hasha, nataka timu hii niipeleke Kombe la Dunia.”

Fainali za Kombe la Dunia, mwakani zitapigwa India ambako kama Serengeti Boys itafuzu kucheza fainali za Afrika na ikaingia nusu fainali kwa maana timu nne bora zote zitashiriki fainali hizo ambazo tayari Tanzania imejiwekea mazingira mazuri ya kufuzu.
“Timu hii nimeanza nayo zaidi ya mwaka mmoja. Sioni kama itakuwa kikwazo kuifanikisha kufika fainali za Kombe la Dunia. Namuomba Mungu atunyooshee mkono wake, nawaombea viongozi wa TFF wazidi kuihudumia timu hii, lakini pia wadau wengine waisapoti timu hii bila kuangalia au kuchagua mtu anayeongoza TFF. Hii ni timu ya Watanzania wote,” amesema Shime maarufu kama Mchawi Mweusi.

BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...