Na Selemani Semunyu - JWTZ
KLABU ya Golf ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ya Lugalo Jijini Dar es Salaam imeahidi kuendeleza Uwanja na klabu hiyo na kuwa na mafanikio makubwa kimataifa ukilinganisha na klabu zingine za Golf na kuwa kitovu cha Michezo na Uchumi kutokana na uwekezaji katika Uwanja huo.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti Mpya wa klabu hiyo Brigedia Jenerali Michael Luwongo wakati akikagua Uwanja wa Klabu hiyo ikiwa ni mara ya Kwanza tangu kuteuliwa na kushika nafasi hiyo Jijini Dar es Salaam.
“Uwanja wa Klabu ya Golf ya Lugalo ndio uwanja wa Kwanza uliojengwa na Wazalendo hivyo tunataka kuhakikisha unakuwa na hadhi ya kimataifa na kuzalisha wachezaji watakaoletea taifa Ushindi” AlIsema Brigedia Jenerali Luwongo.
Brigedia Jenerali Luwongo alisema uwekezaji wenye lengo la kuwa kitovu cha Michezo yote kwa kuwa viwanja bora licha ya kuendeleza michezo lakini inaweza kuwa kitovu cha kiuchumi kutokana na wageni na wazawa kutumia viwanja hivyo vitakavyokuwa na ubora wa Kimataifa.
Mwenyekiti huyo alisema mbali na Uboreshaji Miundombinu kazi kubwa iliyoko mbele yake ni kuhakikisha Mchezo wa golf unachezwa na watu wa rika zote lakini hasa vijana na Watoto ambao watakuwa tegemeo na hazina kubwa kwa Taifa.
Alisema kumekuwa na dhana isiyosahihi kuwa mchezo wa golf ni kwa matajiri dhana ambayo ameipinga na kutaka watu wajitokeze katika Uwanja huo unaomilikiwa na JWTZ ambao gharama za uchezaji wake ni ndogo ukilinganisha na klabu zingine.
“Uwanja ni wa Jeshi lakini sio kwamba Wanajeshi pekee ndio wa naruhusiwa kuja kucheza hata ukiangalia wanajeshi wanaotumia uwanja huo ni ndogo ukilinganisha na raia na wageni toka nje ya Nchi” Alisema Mwenyekiti.
Aidha alitoa Wito kwa Maofisa na Askari wa JWTZ kujitokeza kuwa wanachama katika Klabu hiyo lakjini pia kushiriki mchezo wa Golf.
Kwa upande wake Msimamizi wa Miundombinu wa Klabu hiyo Kanali Mstaafu Jackson Nsigaye amesema sasa wana viwanja 18 ambavyo ndio sahihi vya Golf toka Viwanja Tisa walivyokuwa navyo awali na muelekeo ni kuwa na Viwanja vya michezo mingine pia ili kiwe kituo cha michezo.
Naye Meneja wa Uwanja huo Kanali Omary alisema mpaka sasa ndio uwanja pekee wenye mashindano mengi kuliko vilabu vyote na wataendeleza mafanikio hayo katika mwaka huu.
Brigedia Jenerali Luwongo ameteuliwa kushika wadhifa huo na Mlezi wa Klabu hiyo ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Marehemu Brigedia Jenerali Mstaafu Ernest Galinoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...