Na Teresia Mhagama

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amefanya mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Menejimenti ya TANESCO na kutoa vipaumbele vya kazi ili nchi iweze kuwa na umeme wa uhakika utakaotosheleza mahitaji ya Wananchi.

Kikao hicho kilifanyika jijini Dar es Salaam katika Ofisi za TANESCO ambapo hii ni mara ya Kwanza kwa Profesa Muhongo kufanya kikao na Bodi hiyo kutoka ilipozinduliwa mwezi Mei, mwaka huu.

Katika kikao hicho, Profesa Muhongo aliitaka Bodi hiyo kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo ya upanuzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I, kiasi cha megawati 185 na ujenzi wa mradi wa Kinyerezi ll wa megawati 240.

Aidha aliitaka Bodi hiyo kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kutathmini mapato ya Shirika ikiwemo kupima utendaji kazi wa Mameneja wa TANESCO katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na Kanda.

Alisema kuwa Mameneja hao watapimwa kwa kutumia vigezo vitatu ambavyo ni kuongeza makusanyo ya mapato, kuongeza idadi ya wateja wapya waliounganishwa na huduma ya umeme na ubunifu wa kutatua matatizo ya umeme katika eneo wanayoyasimamia. “ Mfano unakuta nguzo za umeme zinaoza hadi zinaanguka chini na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa wakati kuna Meneja katika eneo hilo la kazi, hii haikubaliki,” alisema Profesa Muhongo.

Kuhusu Majadiliano ya mikataba mbalimbali, Profesa Muhongo aliitaka Bodi hiyo kuhakikisha kuwa majadiliano hayo yanapangiwa muda maalum wa kumalizika na yasichukue muda mrefu.

“Ifike mahala kampuni au mtu aambiwe kama mkataba husika unawezekana au hauwezekani badala ya kuwa na majadiliano ya muda mrefu yasiyokuwa na ukomo, hivyo mikataba ambayo haijakamika, Menejimenti iiwasilishe kwa Bodi. Tunataka ifikapo Agosti 30, 2016 vitu vyote vya zamani viwe vimekamilika ili tuanze masuala mapya,” alisema Profesa Muhongo.

Muhongo alisisitiza kuwa changamoto zilizopo za upatikanaji wa umeme wa uhakika na usambazaji wa nishati hiyo zisimamiwe kwa umakini ili ziweze kutatuliwa ndani ya miaka 3.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe alisema kuwa bado kuna jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa umeme unawafikia wananchi wengi hivyo aliisisitiza TANESCO kufanya kazi kwa ufanisi ili izalishe umeme mwingi na kusambaza kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alex Kyaruzi alisema kuwa maagizo yote ambayo Profesa Muhongo ameyatoa wana uwezo wa kuyatekeleza na kwamba wataisimamia kwa umakini

Menejimenti ya TANESCO ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi unaotakiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Wa Pili kulia), na Bodi na Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Waziri ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, James Andilile na kulia kwa Waziri ni Mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Shirika, Lugano Wilson.
Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ikiwa katika kikao na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ( hayupo pichani) na Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...