Na Lulu Mussa
Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora ameuagiza ungozi wa Dezo Civil Constractors Co. Ltd kuhakikisha ujenzi
wa Miundombinu ya maji taka katika Manispaa za Ilala na Temeke unakamilika
kwa muda uliopangwa na kwa ubora wa hali ya juu kwa kuzingatia makubaliano
yaliyopo katika mkataba.
Akikagua ujenzi
unaoendelea wa miundombinu hiyo, katika Wilaya ya Ilala eneo la Bungoni, Prof.
Kamuzora amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bw. Palela Msongera
kuhakikisha changamoto zinazojitokeza katika ujenzi huo zinatatuliwa mara moja
ikiwa ni pamoja na utupaji wa taka maji na taka ngumu katika mfereji huo
unaojengwa.
Awali Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala Bw. Palela Msongela alimueleza Katibu Mkuu kuhusu
changamoto zinazohusu mazingira hususan uhaba wa miundombinu ya mifumo ya maji
taka na ujenzi wa makazi holela unaosababisha udhibiti hafifu wa taka.
Aidha, Prof.
Kamuzora amewataka watendaji wa Manispaa ya Ilala kuwaelimisha wananchi juu ya
athari zinazoweza kujitokeza kwa kutiririsha maji machafu kuwa ni pamoja na
milipuko ya magonjwa hususan kipindupindu na kuhatarisha afya za wakazi hao.
Kwa upande wake Diwani
wa Kata ya Buguruni Bw. Adam Fugame amemhakikishia Prof Kamuzora kuwa ataongea
na wananchi katika Kata yake na kusisitiza matumizi sahihi ya sheria ndogondogo
za mitaa walizojiwekea ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini wananchi wanaokiuka
taratibu hizo.
“Nikuhakikishie,
kwa kupitia mikutano na vikao na wananchi katika Kata yangu, tutazidi
kusisitiza juu ya jambo hili na kuweka sheria kali zaidi kwa watakao kaidi”.
Alisisitiza Mhe. Diwani Fugame
Ujenzi huo wa Ukuta wa (Obama/Ocean Road na Kigamboni) na
Miundombinu ya maji taka katika Manispaa za Ilala na Temeke unatekelezwa chini
ya Ofisi ya Makamu wa Rais chini ya Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi.
Mradi huu unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP). Kampuni
ya Dezo Civil Contractors ndio inafanya ujenzi huu na unatarajiwa kuzinduliwa
hivi karibuni na kazi zinatarajiwa kukamilika mwezi Julai 2017.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof.
Faustin Kamuzora (kulia) akimsikiliza Diwani wa Kata ya Buguruni Mhe. Adam Fugame (Kushoto) wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi
wa mfereji wa maji taka katika eneo la Ilala Bungoni, Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bw.
Palela Msongela (kushoto) akiongea na
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora mara baada ya
kukagua ujenzi unaoendelea katika mfereji wa kupitisha maji taka eneo la Ilala
Bungoni
Bw. Gervas wa Kampuni ya Dezo Civil
Contractors Co. Ltd akifanunua jambo kwa Prof Kamuzora, Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais, katika eneo la Temeke ambapo Kampuni hiyo imepewa kazi ya
kusafisha na kujenga mfumo wa maji taka. Katikati ni Bw. Motongori Chacha, Afisa
Mazingira Manispaa ya Temeke.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof.
Faustin Kamuzora (kushoto) akimsikiliza Bi. Ukende Mkumbo kutoka Taasisi ya
Mwalimu Nyerere Kigamboni akifafanua hatua za ujenzi wa ukuta katika eneo lao.
Katikati ni mwakilishi kutoka Kampuni ya Dezo Civil Contractors Co. Ltd
Sehemu ya Ukuta wa barabara ya Obama/Ocean Road jijini Dar es salaam ukarabati ukiendelea.(Picha na Habari
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Ofisi ya Makamu wa Rais.)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...