Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kurekebisha Sera na Sheria za kodi ili kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiliamali kupata thamani ya shughuli wanazozifanya.

Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua Mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa Vyakula nchini (TAFOPA) uliofanyika katika ukumbi wa Mwl. Nyerere uliopo Jijini humo.Mama Samia amesema kuwa wafanyabiashara na wajasiliamali nchini wamekuwa wakilalamikia ongezeko la kodi katika bidhaa mbalimbali wanazozizalisha hadi kupelekea kushindwa kuona faida ya shughuli hizo hivyo ni muhimu kwa Serikali kusikiliza kilio chao kwa kutafuta namna bora itakayomaliza tatizo hilo.

“Serikali ya Awamu ya Tano imeliona tatizo hilo na imeahidi kulifanyia kazi kwa kuzipitia upya sheria hizo na kuzifanyia marekebisho ili kila mwananchi atoe kodi bila kinyongo na apate faida ya shughuli anayoifanya,”alisema Mama Samia.Amezitaja changamoto zingine ambazo Serikali itazifanyia kazi ni kujenga miundombinu katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wajasiliamali, kupunguza muda wa upatikanaji wa leseni za biashara pamoja na kuhakikisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa inatenga maeneo kwa ajili ya wajasiliamali hao.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema kuwa jambo analojivunia katika uongozi wake ni kuweza kuwahamasisha Watanzania kuelewa ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo kwa sasa nchi nzima wanazungumzia habari hiyo.“Asilimia kubwa ya wananchi wanazungumzia namna ya kuanzisha viwanda kama sehemu ya kujipatia kipato na ndio maana mikutano ya wajasiliamali imekua ikiongezeka siku hadi siku, hii inaonyesha dhahiri kuwa watanzania wameamua kushirikiana na Serikali katika kuinua uchumi wa nchi kupitia viwanda,”alisema Mwijage.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha TAFOPA, Susan Laizer amefafanua kuwa maeneo yatakapotengwa yatasaidia kupunguza uharibifu wa mazao ya chakula yanayovunwa wakati wa msimu husika pia yatatoa ajira nyingi kwa wananchi watakaokuwa wakifanya shughuli za uzalishaji katika maeneo hayo.“Tunaiomba Serikali yetu itusaidie kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli zetu hadi kwenye sehemu za vijiji ili wakulima wapate soko la bidhaa zao kwa urahisi pamoja na kuepuka madalali wanaozorotesha vipato vyao,”alisema Bi. Susan.

Aidha, Bi Susan amempongeza Mama Samia kwa kuteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa mjumbe wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kwenye jopo la kuwawezesha wanawake kiuchumi kwani ni sifa kwa Taifa na fursa kwa wasindikaji wote nchini.Chama hicho kimeanzishwa rasmi mwaka 1977 baada ya wanawake kupata mafunzo ya usindikaji wa vyakula yaliyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) ikishirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo Duniani (UNIDO). 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...