Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 25
Januari, 2017 amefungua rasmi awamu ya kwanza ya miundombinu na utoaji wa huduma
ya usafiri wa haraka wa mabasi (BRT) katika Jiji la Dar es Salaam uliotekelezwa
kwa lengo la kukabiliana na msongamano wa magari ndani ya Jiji na athari zake
katika shughuli za uzalishaji mali na ustawi wa jamii.
Mradi huu wa
kwanza kutekelezwa Afrika Mashariki na wa tatu Barani Afrika, umehusisha ujenzi
wa Kilometa 20.9 za barabara za Kimara – Kivukoni, Fire – Kariakoo na Magomeni
– Morocco, vituo vya mabasi 27, madaraja ya waenda kwa miguu 3 na vituo vikuu
3.
Awamu hii ya
kwanza ya utekelezaji wa mradi wa miundombinu na utoaji huduma ya usafiri wa
haraka wa mabasi imegharimu Shilingi Bilioni 403.5 ambapo kati yake Shilingi
Bilioni 86.5 zimetolewa na Serikali ya Tanzania na Shilingi Bilioni 317 ni
mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Utekelezaji
wa mradi huu umepangwa kufanywa kwa awamu 6, na awamu ya pili ambayo ipo katika
maandalizi ya kumpata mkandarasi baada ya kupata fedha za mkopo kutoka Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), itahusisha ujenzi wa barabara ya kutoka katikati ya
Jiji – Mbagala, Magomeni – Chang’ombe na Chang’ombe – Jitegemee. Ujenzi huu
utahusisha jumla ya Kilometa 19.3 za barabara na barabara za juu 2 (Flyovers) katika eneo la Chang’ombe na
Uhasibu.
Akizungumza
kabla ya kufungua rasmi awamu ya kwanza ya mradi huu, Mhe. Rais Magufuli
amemshukuru Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa
kuanzisha mradi huo katika kipindi chake cha uongozi, na amewapongeza wadau
wote waliohusika katika utekelezaji ikiwemo Wizara ya Ujenzi na Benki ya Dunia iliyotoa
mkopo huo.
Mhe. Rais Magufuli
ameiomba Benki ya Dunia kuharakisha mchakato wa kutoa fedha za mkopo
utakaowezesha kuanza kwa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara
ya Ubungo (Ubungo Interchange) ili
kuongeza ufanisi wa mradi.
Mhe. Dkt.
Magufuli amesema nia ya Serikali yake ni kuifanya Dar es Salaam kuwa Jiji la
kisasa kwa kuhakikisha inakomesha tatizo la msongamano wa magari ambapo pamoja
na kutekeleza mradi huo pia itajenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kati ya Dar es Salaam na Morogoro na kujenga
barabara za haraka (Express Road) kati
ya Dar es Salaam na Chalinze hivi karibuni.
“Tunataka Dar
es Salaam liwe Jiji la kisasa, ndugu zangu wa Dar es Salaam nataka mniamini
hivyo, hivi karibuni tunapitia tenda na tutapata Mkandarasi wa kuanza kujenga
reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo kuna jumla ya kilometa 200 na
treni zitakazopita zitatumia mafuta na umeme”
“Lakini pia
mchakato wa kujenga barabara ya haraka (Express Road) kutoka Dar es Salaam hadi
Chalinze yenye njia 6 na hatua zote zimekamilika na kilichobaki ni mazungumzo
na wakandarasi kabla ya kuanza kujenga” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais
Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika, kuhakikisha mradi huo unaendeshwa kwa
faida, miundombinu yake inatunzwa vizuri, wananchi wananufaika kama
ilivyokusudiwa na pia ametoa siku 5 kwa Jiji la Dar es Salaam kufanya uamuzi
juu ya matumizi ya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 5.8 zilizotolewa na mbia
anayemiliki asilimia 51 ya hisa za kampuni ya UDA-RT.
Pamoja na
Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali na Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa
na sherehe hizo zimehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya
Afrika Bw. Makhtar Diop ambaye ameipongeza Tanzania kwa kutekeleza mradi huu
muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii na ameahidi kuwa Benki hiyo ipo tayari
kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara
zitakazosaidia kuondoa msongamano wa malori yanayokwenda bandarini kupeleka na kuchukua
mizigo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Januari,
2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Makhtar Diop pamoja na viongozi wengine wakikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji Huduma ya Mabasi yaendayo Haraka katika jiji la Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Makhtar Diop wa kwanza kulia wavivuta kitambaa kuashiria ufunguzi rasmi wa Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji Huduma ya Mabasi yaendayo Haraka katika jiji la Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI George Simbachawene pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiweka kadi ya Kieletroniki katika Mashine ya UDART ilikuweza kupita kama ishara ya Ufunguzi rasmi wa Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji Huduma ya Mabasi yaendayo Haraka katika jiji la Dar es Salaam. Pembeni yake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI George Simbachawene akimuelekeza jambo katika mashine hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia mara baada ya kuendesha gari la Mwendo Kasi katika kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Haraka (BRT) mara baada ya kufungua rasmi Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji Huduma ya Mabasi yaendayo Haraka katika jiji la Dar es Salaam.
ais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipungia mkono pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Makhtar Diop mara baada ya kutoka kukagua moja ya basi linalotumika katika utoaji huduma ya Usafiri wa Haraka (BRT)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...