Shirika la kimataifa la huduma la Rotary nchini Tanzania limezindua mpango maalumu wa miaka mitano wa kuhifadhi mazingira. Mpango huo ulizinduliwa rasmi katika shule ya secondary ya Tambaza jijini Dar es Salaam kwa tukio la upandaji miti 70 katika eneo la shule hiyo hivi karibuni.

Kupitia mpango wa mazingira wa Rotary unaoitwa Rotary Mission Green, shirika hilo limedhamiria kuwekeza katika mazingira kwa kipindi cha miaka mitano kupitia mikakati miwili wa kwanza ukiwa ni kuhamasisha kupunguza matumizi ya nishati itokanayo na miti katika taasisi kubwa kwa kutambulisha nishati mbadala. Na pia kwa kuhamasisha na kushiriki katika zoezi la upandaji miti kwa kushirikiana na serikali za mitaa, mashirika binafsi na jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika tukio hilo, mgeni rasmi ambaye alikuwa Mhe. Prof. Faustin Kamuzora, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira alihakikishia Rotary ushirikiano wa serikali katika utekelezaji wa mpango huu ambao uko sambamba na malengo ya serikali katika uhifadhi wa mazingira.

“Katika ngazi ya serikali tunaahidi Rotary kuwa tutashirikiana nanyi kwa kuwapa msaada wa kiufundi, maeneo, miche, elimu kwa umma na pia ufuatiliaji na tathmini wa mradi. Hivi sasa tunahamasisha wananchi waishi maisha yanayohifadhi mazingira, kila mmoja wetu ana jukumu la kushiriki katika mpango huu sio tu kwa kupanda mti bali kwa kuishi kwa kufikiria mazingira. Elimu kwa umma ni muhimu sana kwa sababu tunaamini kila mmoja wetu akielewa anachotakiwa kufanya katika kuhifadhi mazingira basi atafanya maamuzi yaliyo sahihi akiwa katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku,” aliongeza Mhe. Kamuzora.

Naye kiongozi wa Rotary Gavana Kenneth Mugisha akizungumzia mpango huo wa Rotary alisema kuwa shirika hilo mara zote hujihusisha katika miradi ya kusaidia jamii yenye malengo ya muda mrefu.

“Mpango huu wa Rotary Mission Green ni moja ya miradi mikubwa sana ambayo tumewahi kufanya katika jamii. Hapa Tanzania pekee tunategemea kupanda miti takribani milioni 5 au zaidi na pia kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala. Tunapiga hatua muhimu sana leo hii katika uhifadhi wa mazingira kwa kizazi kijacho cha wajuukuu zetu na watoto wao,” alielezea Rotary Gavana Mugisha.

Kupitia mradi huu Rotary pia itachangia katika uchumi kwa kuwezesha wapandaji miche ya miti ambao miche hiyo itatumika katika mradi na vile vile baadhi ya miti inayopandwa pia kutakuwa na miti inayoweza kutumika katika biashara kama vile za matunda au bidhaa za mbao, na hivyo kuongeza kipato kwa familia na jamii.

Katika mradi wa Rotary wa mazingira, miti itapandwa katika maeneo mbali mbali nchini ikiwemo, pembeni mwa barabara, sehemu za maegesho ya magari, katika taasisi mbali mbali za srikali na binafsi, mahospitali kwa nia ya kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi, kupendezesha mazingira, kupunguza kelele na magonjwa.

Mradi wa Rotary wa mazingira pia unategemea kushirikiana na mashirika na taasisi mbalimbali katika kuwezesha mradi kifedha, au kushiriki kupanda miti katika maeneo yao na watakaohakikisha miti inayopandwa inatunzwa hadi kukua.

Rotary Tanzania imechukua hatua hii ya kuhifadhi mazingira ikiwa kama agizo la Rais wa Rotary Kimataifa Ian Riseley ambaye ameagiza kila mwanachama wa Rotary duniani kote ashiriki kupanda hata mti mmoja na hivyo kuhakikisha katika mwaka huu miti milioni 1.2 inapandwa duniani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...