Na Prof Joseph Mbele
Kampuni ya Ramble Pictures, ambayo inatengeneza filamu, imemaliza kutengeneza filamu inayohusu safari za mwandishi Ernest Hemingway Afrika Mashariki miaka ya 1933-34 na 1953-54. Nilishaandika taarifa za awali kuhusu filamu hiyo katika blogu hii.
Sehemu kubwa ya filamu hii ni mazungumzo baina ya Mzee Patrick Hemingway na mimi kuhusu safari hizo za Ernest Hemingway, falsafa yake juu ya maisha na sanaa. Patrick Hemingway ni moto pekee wa Ernest Hemingway aliye bado hai. Filamu inaelezea mambo juu ya mwandishi Ernest Hemingway ambayo yalikuwa hayafahamiki vizuri, hasa juu ya namna mwandishi huyu alivyoipenda Afrika.
Filamu hii inaitangaza Tanzania, kwa kuwa inaonyesha maeneo kadhaa ya nchi na watu wake, pamoja na safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro. Chimbuko muhimu la filamu hii ni kozi niliyotunga na kufundisha iitwayo Hemingway in East Africa.Nilisafiri na wanafunzi 29 wa chuo cha St. Olaf, ninapofundisha, tukawa tunapita katika maeneo kadhaa ya Tanzania ambamo Ernest Hemingway alipita, huku tukisoma na kujadili maandishi yake kuhusu sehemu hizo.
Wakati filamu hiyo ilipokuwa inatengenezwa, niliweka taarifa mtandaoni, na nilipeleka taarifa sehemu kadhaa katika mfumo wa serikali ya Tanzania, kuelezea kuwa kuhusu filamu hii itakavyoitangaza Tanzania. Nilifarijika kupata ujumbe kutoka Uwakili wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ukiafiki kuwa hii ni "fursa maridhawa ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni" kama nilivyoelezea katika blogu hii.
Filamu inapatikana katika tovuti ya Ramble Pictures.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...