Naibu Waziri wa Madini, Doto Mashaka Biteko ambaye
ameapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya
Madini tarehe 8 Januari, 2018 ameanza kazi rasmi kwa kufanya
kikao na Viongozi na Watumishi wa Wizara husika.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Wizara jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus
Nyongo na Katibu Mkuu, Profesa Simon Msanjila.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri huyo alieleza
kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya viongozi na
watumishi wa Wizara ili kwa pamoja wasimamie ipasavyo
Rasilimali Madini na kuhakikisha kuwa inafaidisha Taifa.
“ Ili kutimiza malengo ya Rais wetu ya kuhakikisha kuwa Rasimali
Madini inaendelezwa ipasavyo, hatuna budi kushirikiana na
kushikamana ili kuwe na umoja utakaoleta ufanisi katika
utekelezaji wa majukumu kwani sisi sote ni watumishi wa
watanzania,” alisema Biteko.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
amesema kuwa Uteuzi wa Naibu Waziri wa Pili katika Wizara ya
Madini unaonesha namna Rais John Magufuli anavyoichukulia
kwa umuhimu wa pekee Sekta ya Madini ambayo ni muhimu
katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
“ Tutashirikiana kwa pamoja na watumishi wa Wizara ili kuweza
kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa mbele zaidi,” alisema
Nyongo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila alisema kuwa viongozi hao na watumishi kwa
pamoja watafanikisha mategemeo na malengo ya Rais John
Magufuli ya kuhakikisha kuwa Rasimali Madini inalinufaisha
Taifa.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaeleza watumishi kuhusu uamuzi wa
Rais John Magufuli wa kutengua uteuzi wa Kamishna wa Madini,
Mhandisi Benjamin Mchwampaka na kumteua Profesa Shukrani
Elisha Manya kuwa Kamishna wa Madini na pia kukaimu nafasi
ya Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini na hivyo kuwaasa
watumishi kumpa ushirikiano Kamishna huyo mpya.
Naibu Waziri Mpya wa Madini, Doto Biteko (katikati) akizungumza katika kikao chake na watumishi wa
Wizara ya Madini. Kulia kwa Naibu Waziri Doto Biteko ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila na kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza katika kikao kati ya Naibu Waziri Mpya wa
Madini, Doto Biteko (katikati) na watumishi wa Wizara ya Madini. Kulia kwa Naibu Waziri Doto Biteko ni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (aliyesimama) akizungumza katika kikao cha
Naibu Waziri Mpya wa Madini, Doto Biteko (katikati) na watumishi wa Wizara ya Madini. kushoto kwa
Naibu Waziri, Doto Biteko ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Madini, wakimsikiliza Naibu Waziri Mpya wa Madini, Doto Biteko
(hayupo pichani) wakati alipowasili katika Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...