Mwandishi Maalum,Bukoba
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina amekamata kilo 65600 za samaki wachanga aina ya Sangara waliokaushwa kwa chumvi wenye thamani ya shilingi milioni mia tatu katika Kisiwa cha Lubili wilayani Muleba kwenye Mkoa wa Kagera baada ya wamiliki wa samaki hao kukimbia.
Akizungumza leo na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera, Mpina amesema tukio la kukamatwa kwa samaki hao lilifanikiwa baada ya yeye kupata taarifa kutoka kwa raia mwema ambapo aliagiza mamlaka za Wilaya ya Muleba kufuatilia kwa karibu hatimaye kuwakuta samaki hao wakiwa wameanikwa chini katika kisiwa hicho.
Waziri Mpina alisema Sheria ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 kifungu cha 90(1) inataka samaki wanaovuliwa waandaliwe katika mazingira yanayokidhi vigezo vya usalama kwa mlaji na kwamba ni kosa kisheria kuwavua au kuchakata samaki aina ya Sangara walio chini ya sentimeta 50 kwa kuwa ni wachanga na sentimita 25kwa Samaki aina ya Sato. Pia sentimita 85 kwa Sangara kwa kuwa ni wazazi wanaotakiwa kundelea kuzaa.
Aidha Waziri aliongeza kwamba Sheria hiyo imetoa mamlaka kwa watendaji wa Serikali kutaifisha mali zote zilitumika katika uvuvi haramu kupitia kifungu cha 37(a) (ii) na (iii) pamoja na Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu namba 29 ya mwaka 1994.
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (katikati )akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bi Mwanaidi Mlolwa akitoa maelezo baada ya kushuhudia shehena ya samaki wachanga aina ya Sangara kilo 65600 mjini Bukoba waliokamatwa katika kisiwa cha Lubili wilayani Muleba leo.Mwenye koti ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustapha Kijuu.

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (aliyenyanyua mikono ) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustapha Kijuu (mwenye koti) leo, nje ya ghala la kuhifadhia samaki katika ofisi ya Uvuvi mjini Bukoba mara baada ya kushuhudia shehena ya samaki wachanga aina ya Sangara kilo 65600 waliokamatwa katika kisiwa cha Lubili wilayani Muleba.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustapha Kijuu (aliyesimama) akisoma taarifa ya mkoa kuhusu sekta ya mifugo na Uvuvi kwa Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (alikaa kulia kwake) leo, mara baada ya kufanya ziara ya ghafla leo ili kushuhudia shehena ya samaki wachanga aina ya Sangara kilo 65600 waliokamatwa katika kisiwa cha Lubili wilayani Muleba. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi nchini, Mwanaidi Mlolwa.
Sehemu ya shehena ya samaki wachanga waliokaushwa kwa chumvi aina ya Sangara kilo 65600 waliokamatwa katika kisiwa cha Lubili wilayani Muleba, wakiwa wamehifadhiwa katika ghala kwenye ofisi ya Uvuvi jijini Bukoba. Samaki hao walikaatwa kufuatia raia mwema kutoa taarifa kwa Waziri Luhaga Mpina hivi karibuni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...