Mkaazi wa kata ya Daudi Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Aloyce Bura amesema alifurahi na kuchinja nguruwe mara baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa Rais John Magufuli amemteua Alexander Mnyeti kuwa mkuu wa Mkoa huo, kwani wananchi wanyonge hivi sasa watakuwa wamepata mtetezi wao. 
 Bura aliyasema hayo mbele ya Mnyeti, wakati akizungumzia kero yake ya kunyang'anywa ardhi yenye makaburi ya familia yake na kigogo wa eneo hilo kwa ushirikiano na ofisa ardhi. Alisema miezi mitatu iliyopita aliposikia kwenye vyombo vya habari kuwa Mnyeti ameteuliwa na Rais Magufuli kuwa mkuu wa mkoa huo, alichinja nguruwe na kusherehekea na ndugu zake. Alisema alichinja nguruwe huyo na kusherehekea na familia yake kwani aliamini wanyonge watapata msaada kama alivyowasaidia wananchi wa Arumeru, wakati akiwa mkuu wa wilaya hiyo. 
 "Mimi nimekaa Arumeru kwa muda mfupi nimesikia sifa za Mnyeti kutetea wanyonge akiwemo kijana aitwaye Nyangusi wa Ngaramtoni alidhulumiwa ardhi lakini alisaidiwa na Mnyeti na kurudishiwa eneo lake," alisema Bura. 
 Alimuomba Mnyeti amsaidie arudishwe eneo lake ambalo lina makaburi ya babu na bibi yake lakini likaporwa na mtu mwenye fedha ambaye alisaidiwa na mmoja kati ya maofisa ardhi wa wilaya hiyo. "Nimefuatilia suala hili kwa muda mrefu hadi ofisi ya ardhi ngazi ya kanda kule Moshi lakini sijapata msaada, tunaomba mheshimiwa mkuu wa mkoa tusaidie kama ulivyowasaidia watu wa Arumeru," alisema Bura. 
 Alisema rushwa imetumika kumuondoa kwenye eneo hilo na yeye kunyimwa haki yake ila kutokana na utendaji kazi mzuri wa Mnyeti, ana matarajio makubwa ya kupatiwa ardhi yake na kuendelea kuimiliki upya. 
 “Haihitaji hata elimu ya shahada kujua kuwa sisi ndiyo tunamiliki eneo hilo kwani hata mtu wa darasa la saba atatambua hilo kwani kuna makaburi ya babu na bibi yetu, tunaomba mkuu wa mkoa utusaidie hilo sisi wanyonge,” alisema Bura. 
 Hata hivyo, Mnyeti alimuagiza mkuu wa kitengo cha sheria wa ofisi yake Peter Mangala kupitia nyaraka za Bura ili kama zinaonyesha ndiye mmiliki halali wa eneo hilo apatiwe haki yake. 
 "Mpe mwanasheria wangu nakala ya hizo nyaraka zako ili azipitie na kuzifanyia kazi na ninakuhakikishia kama haki ni yako utarudishiwa eneo lako bila mashaka wala wasiwasi wowote," alisema Mnyeti.
Aliwataka watumishi wa idara ya ardhi kwenye halmashauri za mkoa huo kufanya kazi zao kwa haki, weledi na hofu ya Mungu kwani kwenye maeneo mengi wananchi wanawalalamikia kuwa wenyewe ndiyo wanaosababaisha migogoro ya ardhi. 
 "Ninyi maofisa ardhi ndiyo mnasababisha wananchi waichukie serikali yao kwani mnachukua virushwa na kupindisha haki sasa mimi nitapambana nanyi nione mwisho wenu kwani mnasemwa sana," alisema Mnyeti.

 Wanawake vikongwe wajasiriamali wa Kata ya Uhuru Mjini Mbulu, wakiwa wamepiga magoti mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, wakimuomba awasaidie wapate ardhi yao walioporwa na mfanyabiashara wa mjini hapo.
 Mkazi wa Kata ya Daudi Wilayani Mbulu, Aloyce Bura akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, juu ya ardhi yake yenye makaburi iliyoporwa na mfanyabiashara wa eneo hilo ambapo miezi mitatu iliyopita aliamua kuchinja nguruwe akifurahia uteuzi wa Rais John Magufuli alioufanya kwa Mnyeti ili awatetee wananchi wa mkoa huo.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa kata ya Nambris Halmashauri ya mji wa Mbulu, kwenye ziara yake ya siku saba ya kujitambulisha, kukagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi na watumishi wa eneo hilo na kusikiliza kero, changamoto na maoni yao.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akikagua msingi wa ujenzi wa nyumba ya walimu wa shule ya sekondari Daudi Wilayani Mbulu.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa mji wa Mbulu kwenye ziara yake ya siku saba ya kujitambulisha, kukagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi na watumishi wa eneo hilo na kusikiliza kero, changamoto na maoni yao.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na viongozi na wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu kwenye eneo la Isale linalotaka kununuliwa na Halmashauri hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...