Na Rachel Mkundai, Tunduma
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere ametishia kuwafutia leseni mawakala wa forodha wanaofanya udanganyifu katika kadhia za wateja wao wanazoziwasilisha katika ofisi za TRA pindi wanapotoa au kuingiza mizigo nchini kwani hizo ni njama za kuwepa kodi.
Bw. Kichere ametoa onyo hilo alipokuwa akizungumza na mawakala wa forodha wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Tanzania na Zambia uliopo katika mji mdogo wa Tunduma mkoani Songwe akiwa katika ziara yake kutembelea mikoa ya nyanda za juu kusini.
Kamishna Kichere amesema kumekuwepo na baadhi ya mawakala wa forodha ambao huwasilisha nyaraka zenye taarifa za uwongo au zinazoonesha idadi pungufu ya bidhaa zilizopo kwenye mizigo tofauti na uhalisia.
“Kusema ukweli sitawavumilia maajenti (mawakala) ambao watakuwa wanaongepea serikali, nitafuta leseni zao, tukiwakamata mnaenda kubumba bumba nyaraka zenye ankara za uwongo, nitafuta leseni” alisisitiza Kamishna mkuu wa TRA.
Hali kadhalika, Kichere amewataka mawakala wa forodha hao kushirikiana na maafisa wa TRA kwa kutoa taarifa sahihi za kadhia za wateja wao ili waweze kukadiriwa kodi stahiki wanayotakiwa kulipa na kuilipa kodi hiyo kwa hiyari kwa kuwa wote ni watanzania wanaoshirikiana kujenga taifa moja.
Nao mawakala wa forodha katika mpaka wa tunduma wameufurahia ujio wa kamishna mkuu na kuahidi kushirikiana na maafisa wa TRA kwa kuwa taasisi hiyo ni kiungo muhimu kati yao na wateja wao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...