Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linapenda kutoa taarifa kwa umma kufuatia tukio la moto
kwenye ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililotokea mnamo
tarehe 09 Aprili, 2018 majira ya saa 1:28 usiku mkoani Dodoma.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa moto huo ulisababishwa na shoti iliyotokana na
Power bank iliyokuwa inatumiwa kuchaji simu. Shoti hiyo ilisababisha kuungua kwa
simu, Power bank, sehemu ya meza na kapeti kitendo kilicholeta moshi mkubwa na
taharuki miongoni mwa Wabunge. Ukiachilia mbali taharuki kwa Waheshimiwa
Wabunge hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokana na moto huo.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji anatoa rai kwa Watanzania wote
kuchukua tahadhari kubwa hasa wanapokua wanatumia vifaa vya kieletroniki ambavyo
kwa sasa vipo katika matumizi hadi katika ngazi ya familia. Moto huzuka tu endapo
kitapatikana chakula cha moto, joto la kutosha na hewa ya oksijeni (fuel, heat and
oxygen).
Sambamba na hayo Kamishna Jenerali anahimiza uzingatiaji wa kinga na tahadhari ya
moto katika maeneo yote. Wamiliki wa maeneo ya umma, binafsi na biashara
wanapaswa kufunga vizimia moto kwa kuzingatia ushauri unaotolewa na Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lipo imara na litaendelea kuwaelimisha Watanzania
kuzingatia kinga na tahadhari ya moto ili kuhakikisha maisha na mali vinakuwa salama.
Imetolewa na;
CGF. Thobias Andengenye
Kamishna Jenerali
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
10 Aprili, 2018
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...