Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu.
Na Veronica Simba - Ngara
Serikali imelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutokana
na utendaji kazi wake mzuri katika kuwapatia watanzania kote nchini
huduma ya nishati ya umeme.
Pongezi hizo zilitolewa hivi karibuni, Aprili 8 mwaka huu, na Waziri wa
Nishati Dkt Medard Kalemani wakati wa hafla ya ufunguzi wa matumizi ya
umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara.
“Nalipongeza Shirika letu la TANESCO. Kwakweli Shirika hili limebadilika
sana kiutendaji, hasa katika Menejimenti na wafanyakazi. Wanafanya kazi
kwa kujituma. Baadhi ya watu walizoea kulibeza Shirika hili lakini
wanajitahidi sana kwa sasa,” alisema Waziri.
Waziri alisema kuwa kazi ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati ni
kulisimamia Shirika hilo ili liendelee kufanya kazi nzuri kwa manufaa ya
wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu.
Akizungumzia Mradi huo wa kuiunganisha Ngara na umeme wa Gridi ya
Taifa, Waziri Kalemani alisema kuwa ni wa manufaa makubwa kwani
utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji na hivyo
kuliongezea shirika uwezo zaidi wa kuwahudumia wananchi.
“Kwa kutumia mafuta, Uniti moja ilikuwa inawagharimu TANESCO shilingi
578 wakati huu wa Gridi utawagharimu shilingi 154 tu kwa Uniti,”
alifafanua.
Waziri aliwataka watendaji wa TANESCO kuhakikisha wanawahudumia
wana-Ngara na watanzania wote kwa ubora zaidi kutokana na uwepo wa
umeme wa Gridi ya Taifa katika maeneo mengi zaidi na kuondokana na ule
wa mafuta ambao una changamoto kadhaa.
Aidha, Dkt. Kalemani alibainisha kuwa, sambamba na zoezi la kuhakikisha
Tanzania nzima inaunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa, pia Serikali
inaendelea kupeleka umeme vijijini kupitia miradi inayotekelezwa kupitia
Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Alisema kuwa, kufikia mwaka 2020, hakuna kijiji kitakachobaki bila kuwa na
umeme.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera, Mhandisi Francis Maze akiwasilisha taarifa ya Mkoa wake kwa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, wakati wa hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu.
Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John
Magufuli kwa dhamira yake ya dhati katika kuhakikisha inawaondolea
watanzania kero na changamoto mbalimbali ikiwemo ya umeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito
Mwinuka pamoja na kumuunga mkono Waziri kwa kuipongeza Serikali ya
Awamu ya Tano; aliipongeza Wizara ya Nishati inayoongozwa na Dkt
Kalemani ambayo alisema ndiyo msimamizi mkubwa wa shughuli
zinazotekelezwa na shirika hilo. Alisema kuwa, kwa kuiunga Ngara na umeme wa Gridi ya Taifa, kiasi
kikubwa cha fedha kitaokolewa. “Kwa harakaharaka, tutaweza kuokoa
takribani shilingi bilioni mbili kwa mwaka baada ya kuzima mitambo hii ya
mafuta.”
Aliongeza kusema kuwa TANESCO itaendelea kuzima vituo vya mafuta
sehemu mbalimbali nchini ambapo itasaidia kupunguza gharama za kufua
umeme kwa kutumia mafuta.
Awali, akiwasilisha taarifa ya TANESCO kwa Mkoa wa Kagera, Meneja
wake, Mhandisi Francis Maze alisema kuwa kabla ya kuunganishwa
kwenye Gridi ya Taifa, Wilaya ya Ngara ilikuwa ikitumia umeme wa mafuta
ambapo mahitaji ya juu kwa Wilaya hiyo ni megawati 1.38.
Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Leyla Muhaji akifurahia ngoma
pamoja na kikundi cha burudani kilichokuwa kikitumbuiza wakati wa hafla
ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili
8 mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...