Na Stella Kalinga, Simiyu

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu amefanya ziara mkoani Simiyu Oktoba 03, 2018 na kuzungumza na viongozi wa mkoa huo, ambapo ameeleza kuwa moja ya malengo ya ziara yake ni kufahamu Mipango na Fursa za Uwekezaji zilizopo mkoani Simiyu, ili aweze kuzungumza na wawekezaji nchini Kenya kuwekeza mkoani humo.

Balozi Kazungu amesema nchi ya Kenya ndiyo inaongoza kuwekeza nchini Tanzania ukilinganishwa na nchi nyingine za Afrika ambapo hadi sasa imewekeza takribani dola za Kimarekani bilioni 1.6 hapa nchini.“ Nimekuja hapa ili tufahamiane vizuri, nijue mipangilio yenu, fursa za uwekezaji ziko wapi ili tuweze kuzungumzana wenzetu wakaja kuwekeza, Kenya ni nchi inayoongoza kwa kuwekeza nchini Tanzania, hadi sasa imewekeza takribani dola bilioni 1.6 ” alisema Balozi Kazungu.

Aidha, ameomba ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uendelee kuimarishwa kwa lengo la kuzifanya nchi hizi kuwa shina la viwanda na uwekezaji na kuwa wanufaika wa soko la pamoja la Afrika hali itakayochangia kuimarisha uchumi wa nchi hizo.Pamoja na ushirikiano katika masuala ya uwekezaji na viwanda Balozi Kazungu amesisitiza masuala ya ujirani mwema, upendo na ushirikiano wa kindugu baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo inakaribisha sekta binafsi na iko tayari kutoa ardhi bure kwa wawekezaji walio tayari kuwekeza Simiyu katika maeneo yanayojibu mahitaji ya mkoa na nchi kupitia malighafi zinazolishwa ndani ya mkoa na ndani ya nchi.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akimkabidhi Nakala ya Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu, wakati wa ziara yake mkoani humo, Oktoba 03, 2018.
Kutoka kulia Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini, Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu na Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery kilichopo Bariadi, Bw. Boaz Ogola wakiteta jambo, wakati wa ziara ya Balozi huyo mkoani Simiyu, Oktoba 03, 2018.
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu , Mjini Bariadi wakati wa ziara yake mkoani humo, Oktoba 03, 2018.
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu ( wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mkoa wa Simiyu mara baada ya kuhitimisha ziara yake mkoani Simiyu, Oktoba 03, 2018.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...