Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan.
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi Mkoani Pwani leo oktoba 24 ambapo atatembelea miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari .
Ndikilo amesema ,makamu wa Rais akiwa mkoani humo atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya nne za mkoa huo na ataanzia ziara kwa kukagua miradi ya maendeleo ya Wilayani Bagamoyo.
"Miradi hiyo ni pamoja na kutembelea mradi mkubwa wa Bandari mpya ya Mbegani wilayani Bagamoyo yenye ubia na nchi tatu za Tanzania,Oman na China," alisema Ndikilo.
Amesema kuwa baada ya kukagua miradi wilayani Bagamoyo atakwenda Halmashauri ya wilaya ya Chalinze ambako atakagua miradi ya maendeleo.
"Baada ya hapo atakwenda , Wilaya ya Kisarawe, Mkuranga na atahitimisha ziara hiyo wilaya ya Kibaha"
Aidha mradi mwingine wa kitaifa ni atakaotembelea ni ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) kwenye karakana kubwa iliyoko Soga wilayani Kibaha.
"Mbali ya kutembelea miradi hiyo mikubwa pia atatembelea miradi mingine ikiwemo ya miradi ya afya, maji na elimu,"alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa akiwa wilayani Kibaha Makamu wa Rais anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonyesho ya wiki ya viwanda itakayozinduliwa Oktoba 29 katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika eneo la Picha ya Ndege.
Makamu wa Rais atakapoanza ziara hiyo atapokea taarifa kutoka Halmashauri zote za mkoa huo pia atapata nafasi ya kuzungumza na Wakurugenzi wa Halmashauri hizo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...