Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeunga mkono kwa vitendo kampeni iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kulifanya jiji la Dodoma kuwa kijani kwa kupanda miti katika ofisi yake inayojengwa Ihumwa jijini Dodoma kwenye mji wa serikali.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro mara baada ya watumishi wa ofisi yake kukamilisha zoezi la upandaji wa miti katika mji wa serikali Ihumwa, eneo ambalo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inajengwa ili kutoa huduma kwa umma. Dkt. Ndumbaro amesema kuwa, zoezi la upandaji wa miti katika eneo hilo ni endelevu na kuongeza kuwa, Ofisi yake itahakikisha miti hiyo inatunzwa kwa kuimwagilia maji ili hatimaye kuwe na mandhari ya kijani pindi ofisi yake itakapokamilisha ujenzi wa jengo kubwa.

Naye, mmoja wa watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Menyeaichi Koka ameongeza kuwa, watumishi wa Ofisi ya Rais – Utumishi wameitikia wito wa Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kupanda miti ili kulifanya jiji la Dodoma kuwa kijani na kuishukuru menejimenti ya ofisi kwa kusimamia vema zoezi hilo ambalo kila mtumishi amelifanya kwa hiyari na kwa moyo mkunjufu.

Bi. Koka ahaidi kuwa, atahakikisha mti alioupanda anauhudumia vizuri kwa kuumwagilia maji ya kutosha ili uweze kustawi vizuri na kuwa ni miongoni mwa miti iliyopandwa na kufanikiwa kukua vizuri na hatimaye kuchangia jiji la Dodoma kuwa kijani.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni za kulifanya jiji la Dodoma kuwa kijani Julai 21, 2017 kwa kuongoza zoezi la upandaji wa miti ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kwa vitendo uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamishia Makamo Makuu ya Nchi kutoka Dar es Salaam kuja jijini Dodoma.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza kuhusu ofisi yake kuunga mkono kwa vitendo kampeni ya kulifanya jiji la Dodoma kuwa la kijani iliyozinduliwa na  Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan mara baada ya watumishi wa ofisi yake (hawapo pichani) kukamilisha zoezi la upandaji miti katika ofisi inayojengwa Ihumwa kwenye mji wa serikali jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Mathew Kirama akishiriki katika zoezi la upandaji miti Ihumwa katika mji wa serikali jijini Dodoma, eneo ambalo Ofisi ya Rais-Utumishi inajengwa ili kutoa huduma kwa umma.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Musa Joseph akishiriki kuchimba mashimo kwa ajili kupanda miti Ihumwa katika mji wa serikali jijini Dodoma, eneo ambalo Ofisi ya Rais-Utumishi inajengwa ili kutoa huduma kwa umma.

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakiwa tayari kupanda miti katika ofisi inayojengwa Ihumwa kwenye mji wa serikali jijini Dodoma ili kuunga mkono kwa vitendo kampeni ya kulifanya jiji la Dodoma kuwa la kijani, iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan Julai 21,2017. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...