Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mwita Waitara amezitaka Halmashauri zote kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima kwenye Halmashauri zao bila ya kutumia kisingizio cha ukosefu wa bajeti za kufanya vikao vinavyohusu utoaji wa majina ya mitaa
“Suala la gharama halipo, tumieni vikao vyenu vya kawaida, vya kisheria kutaja majina ya mitaa, suala la anwani za makazi na postikodi iwe ajenda mahususi ya ulinzi na usalama”, amefafanua Waitara
“Wakurugenzi wote wa Halmashauri zote nchi nzima waliopo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI wahakikishe kwamba wanatoa maelekezo mahususi kwa watendaji wote na kuhakikisha kuwa wanatoa majina ya mitaa,” amesema Waitara. Pia amewaelekeza Makatibu Tawala wote Tanzania Bara wahakikishe Halmashauri zote zinatekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi
Waitara ameongeza kuwa mpango huu unatuwezesha kujitambua na kuwatambua watu wetu wanakoishi, na nini kilichowaleta eneo hilo kama ni biashara, uwekezaji na ni muhimu kwa ulinzi na usalama wa raia. Pia amesema kuwa suala la anwani za makazi na postikodi litawasaidia viongozi wao wenyewe kuwatambua wananchi, kuwezesha ukusanyaji wa kodi na kufikisha huduma za Serikali kwa wananchi
“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anataka watanzania walipe kodi, jambo hili likitekelezwa, watanzania watalipa kodi na mpango huu wa kuwatambua wananchi utasaidia kuongeza mapato ambayo yataleta maendeleo ya taifa letu na kujenga miundombinu ya barabara, huduma za afya na elimu,” amesema Waitara.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwita Waitara wakiwa wanatoka kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Sengerema (hayupo pichani) wakati wa ziara yao wilayani humo ya utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwita Waitara akizungumza na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Sengerema na Buchosa (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi wakiwa Nyehunge, Mwanza. Wa tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, wa tatu kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi na wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Sengerema na Buchosa (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi yaliyofanyika Nyehunge, Mwanza. Wa nne kushoto ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara na pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara (wa tatu kushoto) kuhusu kituo cha telesenta wakati wa ziara yao Wilayani humo
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi James Kilaba akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara (wa pili kushoto) kuhusu kituo cha telesenta wakati wa ziara yao wilayani Sengerema. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuel Kipole.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...