Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema wakati Serikali inatarajia kufanya  marekebisho ya Mishahara kwa Wafanyakazi wake wenye uzoefu na makundi mengine ambayo hayakunufaika na nyongeza za Mishahara iliyopita,  Shilingi Bilioni Nne  zimetengwa kwa lengo la kuwapatia Mikopo Vijana ili waweze kujiajiri.
Alisema sambamba na Fedha hizo Serikali ya Abudhabi kupitia Mfuko wa Khalifa {Khalifa Fund} itatoa Shilingi Bilioni 23 kwa Zanzibar kwa ajili ya kusaidia tataizo la ajira kwa Vijana wa Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa 14 wa Baraza la Tisa la Wawakilishi lililojadili Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2019/2020 uliokuwa ukifanyika katika Ujumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. 
Alisema kupatikana kwa Fedha hizo kunatokana na ziara aliyoifanya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohjamed Shein katika Nchi za Falme za Kiarabu mwishoni mwa Mwaka jana.
Alieleza katika kutekeleza azma hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia baadae itaongeza kiasi kama hicho kitakachotolewa na Mfuko wa Khalifa wa Abudhabi ili kusaidia Miradi ya Vijana Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali imekuwa ikichukuwa hatua mbali mbali ili kuhakikisha Vijana wake wanapata ajira, ikielewa ukubwa wa tatizo hilo ambalo ni changamoto wa Dunia ikiwemo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Balozi Seif alitoa wito kwa Vijana hasa wale wanaomaliza vyuo Vikuu na Elimu ya Sekondari kujikusanya pamoja katika kubuni au kutafuta Mradi wa kufanya ili kuitumia vyema fursa iliyopo.
Akizungumzia suala la Ardhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaomba Watendaji wote waliopewa dhamana ya usimamizi wa Sheria za Ardhi wawe Wazalendo kwa kutumia Taaluma zao ili kutatua migogoro ya Ardhi iliyopo kuanzia Shehia, Wilaya, Mikoa hadi Taifa kwa ujumla.
Alisema Zanzibar kwa sasa ina Sheria Tisa zinazohusiana na matumizi bora na endelevu ya Ardhi lakini bado kumejitokeza baadhi ya Viongozi, Watendaji wa Serikali na baadhi ya Watu kuendelea kutoziheshimu sheria hizo.
Balozi Seif  Ali Iddi alisema wahusika hao wamekuwa na tabia ya kuwa madalali wa kuuza au kuchukuwa Ardhi bila ya kufuata Sheria na taratibu zilizopo hali inayosbabisha dhulma na migogoro mingi katika Jamii.
Balozi Seif  alionya kwamba Serikali haitomvumilia na itamchukulia hatua kali Mtu ye yote atakayekuwa na tabia ya udalali au kuhodhi Ardhi kwa utashi wake na kwenda kinyume na Sheria za Nchi zilizopo.
Aliwaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wananchi wote wa Zanzibar kutambua kwamba Ardhi ni Rasilmali muhimu katika Maendeleo ya Taifa na Wananchi wake Kiuchumi na Kijamii.
Balozi Seif alisema  kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Zanzibar, Rasilmali hiyo itawendselea kuwa Mali ya Serikali. Hivyo Wananchi na Taasisi za Umma zitapewa Ardhi kwa matumizi yao tu na haitoruhusiwa kuuzwa, kurithi, kugaiana au kupeana kwa namna ye yote ile bila ya utaratibu na amri itakayotolewa na Serikali kwa mujibu wa Sheria.
Alifafanua kwamba Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 kifungu cha 23{4} imeeleza wazi kuwa:- kila Mzanzibari ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi, kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na Umoja wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alieleza kwamba Serikali Kuu inatambua kuwa wapo baadhi ya wanaojiita Wawekezaji wa Kizalendo wanaoomba na kupewa Ardhi na badala yake huitumia Ardhi hiyo kwa kuinadi sokoni na kuiuza kwa fedha nyingi za Kigeni jambo ambalo halikubaliki na Dola haitasita kuwanyang;’anya ardhi wale watakaobainika kuendeleza vitendo hivyo viovu vinavyohujumu Uchumi.
Alisema hatua mbali mbali zitaendelea kuchukuliwa na Serikali katika kupunguza au kuondosha kabisa migogoro ya Ardhi ikiwemo kuimarisha Mahkama ya Ardhi Nchini pamoja na kuendeleza hatua ya maandalizi ya upimaji wa Miji Mipya Unguja na Pemba.
Balozi Seif alifahamisha kwamba hatua hiyo itakwenda sambamba na utoaji wa Elkimu watakayopatiwa Wananchi juu ya utekelezaji wa Sheria na Miongozo inayotolewa juu ya usimamizi wa matumizi mazuri ya Rasilmali ya Ardhi hapa Nchini.
Kuhusu suala la Mafuta na Gesi asilia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Wataalamu walikuwa akiendelea na hatua ya kuzichambua data na viashiria vilivyopatikana kutokana utafiti wa Rasilmali hiyo.
Alisema zoezi hilo liko ukingoni kumalizika na ifikapo Mwezi Septemba Mwaka huu matokeo ya Utafiti huo yatakabidhiwa rasmi Serikalini na baadae kama alivyotoa ahadi Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein yatatangazwa kwa Wananchi hadharani.
Alitoa wito kwa Wananchi waote kuendelea kuwa wastahamilivu na wazidishe dua zao ili majibu ya utafiti huo yawe mazuri na ishaallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu yatakuwa mazuri kama yanavyotarajiwa na Umma wote Nchini.
Alisema Kampuni ya Utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia ya Ras AL Khaimah {Rak Gas}  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilitiliana saini mkataba wa kufanya utafiti wa uwepio wa Mafuta na Gesi Asilia katika Vitalu vya Zanzibar mnamo Tarehe 23 Oktoba Mwaka 2018.
Aliwakumbusha Wajumbe wa Baraza l;a Wawakilishi kurejea katika Majimbo yao ili wakatimize Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 pamoja na ahadi nyengine walizowaahidi Wananchi wao.
Alisema ni vyema kwa Wajumbe hao wawatendee matendo mema wale wanaowaongoza na kuwasimamia ili na wao wakumbuke fadhila za matendo hayo katika wakati ujao.
Alieleza katika kuharakisha na kuimarisha maendeleo ya Majimbo ya Uchaguzi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeshatoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa Majimbo yote 54 yaliyopo Unguja na Pemba.
Balozi Seif aliwataka Wawakilishi hao kushirikiana na Kamati zao katika matumizi ya Fedha sambamba na usisitizaji wa kufanya marejesho kwa wakati ili taratibu za kupata fedha za awamu nyengine ziweze kufanyika mapema.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar  limeahirishwa hasi Jumatano ya Tarehe 18 Septemba Mwaka 2019.
  1.  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...