Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
BALOZI mdogo wa Jamhuri ya watu wa China Xie Xiuowu amesema nchi yake
itaendeleza azma yake ya kuisaidia Zanzibar katika nyanja tofauti
ikiwemosekta ya afya ikiwa ni juhudi zake za kukuza uhusiano miongoni
mwa nchi hizo mbili.
Alisema misaada wanayoitoa inaongozwa na dhamira njema hasa kwa watu
wenye mahitaji ili kuona nao wanaendelea kufurahia maisha yao ya kila
siku.
Balozi Xie aliyasema hayo katika hafla ya kuwaaga madaktari wa China
wanaomaliza muda wao na kuwakaribisha madaktari wapya ambao nao
watahudumu katika sekta ya afya Zanzibar kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Alikumbusha kuwa Jamhuri ya Watu wa China ilianzisha utaratibu wa
kuleta madaktari Zanzibar tokea mwaka 1964 na utaratibu huo
unaendelezwa na kuimarishwa zaidi hadi sasa.
Alisema kwa sasa wanatekeleza mradi wa kupambana na kichocho, saratani
ya shingo ya kizazi na kuwajengea uwezo watendaji katika sekta ya
tofauti ili kuimarisha uhusiano kati ya Zanzibar na China.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed alisema
uhusiano wa China na Zanzibar unaendelea kuimarika siku hadi siku na
kuiomba China ifikirie namna ya kuwafanya madaktari hao kutumia muda
wa miaka miwili Zanzibar badala ya mmoja ili kutoa huduma zaidi.
Alisema kupitia uhusiano huo China imeweza kuimarisha ujenzi wa
miundombinu ikiwemo hospital ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba.
Aidha aliongeza kuwa wataalam wanaokuja kutoka China husaidia pia
huwaongezea ujuzi wananchi na madakri wa Zanzibar kupitia programu
mbali mbali ikiwemo za televisheni na hospitalini.
Waziri Hamad aliwashukuru kupitia mradi wa kupambana na maradhi ya
kichocho ambapo dola za Marekani Milioni 5 walizotoa zitasaidia
kupambana na maradhi ya Kichocho Zanzibar.
Alisema pesa hizo pia zitatumika katika programu ya miaka mitano ya
kupambana na maradhi ya saratani ya shingo ya mlango wa kizazi kwa
wanawake wa Zanzibar.
“Kiujumla misaada wanayoitoa ndugu zetu hawa ni mingi sana na
hawajawahi kutuwekea masharti yanayotubana, tunashirikiana nao vyema
tofauti na misaada ya nchi nyingine”, alibainisha Waziri Hamad.
Aidha Hamad aliwasifia madaktari hao kwa nidhamu ya kazi ambayo
inapaswa kuigwa na madaktari wazalendo ikiwemo ya kuwahi kazini mapema
bila ya malalamiko yoyote.
“Hili la nidhamu ya kazi kwa kweli sisi kama Wazanzibari na Watanzania
kwa ujumla tunapaswa tuige. Wanawahi kazini na kuondoka kwa wakati na
husikii wakipewa lawama na wananchi wanaowahudumia”, alisema Waziri
Hamad.
Kuhusu timu ya madaktari wapya, Waziri Hamad alisema waliokuja ni
wataalamu zaidi ambao pia watatumika kutoa elimu katika ngazi za vyuo
vikuu vya Zanzibar.
Akitoa salamu za shukran kwa niaba ya wenzake Mkuu wa madakrari
waliomaliza muda wao Dk.Zhang Zhen ameishukuru Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa ukarimu wao waliouonesha katika kipindi chote cha
kuhudumia wananchi Zanzibar.
Alisifia mazingira safi ya visiwa vya bahari ya Hindi ikiwemo Zanzibar
ambavyo vitaendelea kubaki katika kumbukumbu zake.
Nae Kiongozi wa timu mpya ya madaktari hao Dk. Yang Xiaodong aliahidi
kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na weledi ili kutimiza malengo
yaliyokusudiwa.
Balozi mdogo wa China Xie Xiuowu msitari wa pili waliokaa na Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed kushoto kwake wakiwa katika Picha ya pamoja na Timu ya Madaktari wnaomaliza muda wao wa mwaka mmoja kutoa huduma kwa wananchi wa Zanzibar.
Balozi mdogo wa China Xie Xiuowu katikati na Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed kushoto kwake, wakiwa katika Picha ya pamoja na Timu ya Madaktari wapya kutoka China ambao watakuwa wakifanya kazi ya kuhudumia wagonjwa kwa kipindi cha mwaka mmoja Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid akibadilishana mawazo na Balozi mdogo wa China Xie Xiuowu wakati wa hafla ya kuwaaga Madaktari wanaomaliza muda wao na kuwakaribisha madaktari wapya kuhudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hafla hiyo ilifanyika Ubalozi mdogo wa China mjini Zanzibar
Balozi mdogo wa China Xie Xiuowu akitoa hotuba yake katika Hafla maalum ya kuwaaga Madaktari kutoka China wanaomaliza muda wao na kuwakaribisha Madaktari wapya watakaohudumia wananchi kwa kipindi cha Mwaka mmoja. Hafla hiyo ilifanyika Ubalozi mdogo wa China mjini Zanzibar
Waziri wa Afya Hamad Rashid akitoa hotuba yake katika Hafla maalum ya kuwaaga Madaktari kutoka China wanaomaliza muda wao na kuwakaribisha Madaktari wapya watakaohudumia wananchi kwa kipindi cha Mwaka mmoja. Hafla hiyo ilifanyika Ubalozi mdogo wa China mjini Zanzibar
Kiongozi wa Timu ya Madaktari wa kutoka China waliomaliza muda wao wa kuhudumu katika sekta ya Afya Zanzibar akitoa neno la shukran katika hafla maalum ya kuagwa kwao na kukaribishwa kwa Madaktari wapya. Hafla hiyo ilifanyika Ubalozi mdogo wa China mjini Zanzibar
Kiongozi wa Timu ya Madaktari wapya kutoka China Dkt.Yang Xiaodong akitoa nasaha zake katika hafla ya kuagwa na kukaribishwa kwa madaktari hao ambao watahudumu Zanzibar katikakipindi cha mwaka mmoja.
Baadhi ya Madaktari wa kutoka China waliohudhuria katika Hafla
maalum ya kuwaaga Madaktari wanaomaliza muda wao na kukaribishwa kwa
Madtari wapya watakaotoa huduma mbalimbali ikiwemo upasuaji na
Kichocho. Hafla hiyo ilifanyika Ubalozi mdogo wa China mjini Zanzibar
Picha na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...