Na Said Mwishehe, Michuzi TV
TAASISI ya Action Network Tanzania inayojihusisha na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi imewakuwakutanisha wadau wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali za mitaa kutoka Wilaya ya Chalinze na Bagamoyo mkoani Pwani kwa lengo la kutafuta mbinu ambazo zitachochea matumizi ya nishati jadidifu na mbinu za kuweza kupatikana chakula cha kutosha.
Wadau hao wamekutana wilayani Bagamoyo ambapo pamoja na mambo mengine wametumia mafunzo maalumu ambayo yameandaliwa na Climate Action Network Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na wametumia nafasi hiyo kueleza kwa kina mbinu ambazo watazitumia kuhamasisha jamii katika matumizi ya nishat ijadidifu.
Pia wameeleza kuwa, kuna kila sababu ya kuhakikisha kunakuwa na elimu ya kutosha kwa jamii katika kueleza umuhimu wa kutumia nishati mbadala na kutafuta mbinu zitakazosaidia upatikanaji wa chakula cha kutosha huku wakiiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupata sera ambayo itajikita katika kuisimamia na kuindeleza nishati jadidifu nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa majadiliano hayo, Meneja Rasilimali na Ukutanishi Jophillen Bejumula amesema kuwa wana imani kuwa baada ya kukutana na wadau hao kwa majadiliano wanaamini watatoka na mbinu mbadala na kuangalia mbinu gani zitafaa na Serikali isaidie wapi katika kuwasaidia wavuvi, wakulima na wafugaji ikiwa ni sehemu ya makati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Pia amesema kuwa Chalinze na Bagamoyo wananchi wengi wanajishughulisha na kilimo, uvuvi na ufugaji na ni miongoni mwa maeneo ambayo mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha athari kwa namna moja au nyingine.Hivyo kupitia majadiliano hayo watatoka na mbinu za kukabiliana na mabadiliko hayo ikiwemo ya kutumia nishati jadidifu na kuongeza uzalishaji wa chakula.
Wakati huo huo amesema kupitia majadiliano hayo wanajaribu kuonesha changamoto zilizopo katika kuitumia nishati jadidifu na katika hilo wanaona iko haja ya kuwa na mkakati madhubuti kuendeleza matumizi ya nishati jadidifu pamoja na malengo ya muda mrefu.
Bejumula amesema kupitia majadiliano hayo pia wamekumbushwa wajibu wao huku akieleza kwamba Climate Action Network Tanzania wapo katika kuipitia upya sera ya nishati iliyopo na kisha wataandaa majadiliano mazuri na ujumbe wake utawasilishwa Wizara ya Nishati.
"Tunatarajia kuona uwepo na mkakati wa muendelezo wa kuendeleza nishati jadidifu.Tunao ushirikiano mzuri na wakaribu na viongozi wa ngazi za juu Serikali, wamekuwa wakitoa maelekezo nasi tunayafanyia kazi, na tutaendelea kuwasikiliza.Hata hivyo tunadhani ni vema kukawa na sera inayohusu kuendeleza nishati jadidifu nchini Tanzania,"amesema.
Kwa upande wake mmoja ya watoa mada kwenye majadiliano hayo , Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Marian Dk.Brown Gwambene amesema kikubwa ambacho wamekifanya ni kuwasiliza zaidi wadau ambao ndio walengwa na kupitia wao wameibua mambo mapya na hivyo kwa pamoja sasa watakuwa na uelewa wa namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mmoja wa washiriki katika majadiliano hayo Mtafiti na Mhadhiri mstaafu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Hilda Kiwasila amesema umefika wakati wa kuwa na mikakati endelevu katika eneo la nishati jadidifu na kufafanua kuwa Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikiwekeza katika nishati jadidifu lakini tatizo ni kwenye usimamiaji na uendelezaji.
Mshiriki mwingine wa majadiliano hayo kutoka jamii ya wafugaji Monica Sambingu amesema mabadiliko ya tabia nchi yameathiri sana jamii ya wafugaji na kupitia majadiliano hayo atakuwa mabolozi wa kuhamasisha jamii yake kushiriki kukabiliana na athari za mabadiliko hayo ikiwa pamoja na kuhakikisha hakuna uharibifu wa mazingira.
Yanasia Nguma kutoka Idara ya Mifugo na Uvuvi Bagamoyo akizungumza wakati wa majadiliano hayo
Meneja Rasilimali na Ukutanishi kutoka Taasisi ya Climate Action Network Tanzania Jophillene Bejimula akifafanua jambo kuhusu lengo la kuwakutanisha wadau kujadili kuhusu matumizi ya nishati jadidifu pamoja na mbinu mpya katika kuongeza uzalishaji chakula
Mshiriki kutoka jamii ya wafugaji Monica Sambingo akitoa maoni yake kwenye baraza la majadiliano lililoandaliwa na Taasisi ya Climate Action Network Tanzania ili kujadili mabadiliko ya tabianchi
Washiri wakifuatilia majadiliano wakati wa semina maalum iliyowakutanisha wadau wa kada mbalimbali katika Wilaya ya Chalinze na Bagamoyo kujadili athari za mabadiliko ya tabianchi
Washiriki wakifuatilia majadiliano yaliyohusu kutafuta mbinu mpya za kuongeza uzalishaji chakula na utumiaji wa nishati jadidifu kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi
Baadhi ya washiriki wa majadiliano yaliyohusu kuangalia mbinu mpya zitakazosaidia kuongeza upatikanaji wa chakula na matumizi endelevu ya nishati jadidifu .Majadiliano hayo yamefanyika kwa kuwashirikisha wadau kutoka Chalinze na Bagamaoyo na yameandaliwa na taasisi ya Climate Action Netwrok Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...