Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepewa pongezi na Wakazi wa Mkoa wa Lindi kwa kuwaletea huduma ya kivuko cha MV Kitunda kinachofanya safari zake kutoka Lindi kwenda ng’ambo ya pili katika eneo la Kitunda.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni wakati Maafisa Habari wa Idara ya Habari – MAELEZO walipotembelea eneo la feri ambapo kivuko hicho kinafanyia kazi ili kujionea utendaji kazi wa kivuko hicho.
Mfanyabiashara na mkazi wa Kitunda, Yusuph Yahya amesema kuwa kabla ya kivuko hicho biashara zilikuwa ngumu kwa sababu uvushaji wa mizigo haukuwa rahisi pia gharama na muda uliokuwa ukitumika kuvusha mizigo hiyo ni kubwa hivyo muda mwingine wafanyabiashara walikuwa wanapata hasara kutokana na mizigo yao kuharibikia njiani wakati wa usafirishaji.
“Kwa kweli tunamshukuru sana Rais wetu Magufuli kwa kutuletea kivuko hiki kwani mwanzoni tulikuwa tunatumia usafiri wa boti ndogo ndogo hata magari ilikuwa shida kuyavusha lakini kwa sasa usafiri ni salama biashara zimekuwa zikifanyika kwa urahisi hata gharama za usafirishaji zimeshuka, zamani mzigo mdogo tu unasafirsha zaidi ya shilingi 2000 hadi 3000 lakini sasahivi tunavusha mzigo mdogo kuazia shilingi 1000,” alisema Yahya.
Naye Mkazi wa Manispaa ya Lindi, Shakira Nandonde amesema kuwa kivuko hicho kimewaondolea adha ya usafiri hasa kwa wanawake, watoto na walemavu kwa sababu boti zilikuwa zikipaki mbali na nchi kavu hivyo ilikuwa ni changamoto kuufikia usafiri huo pia kwa wagonjwa ilikuwa changamoto kuwatoa Kitunda kuwaleta Lindi Mjini ambako ndio kuna matibabu makubwa.
Mkazi mwingine wa Kitunda, Said Omary ameishukuru Serikali kwa ujio wa kivuko hicho kwani kimepunguza gharama za usafiri kutoka shilingi 500 malipo ya usafiri wa boti mpaka shilingi 300 kwa usafiri wa kivuko pia kivuko hicho kimesaidia kupanua mji wa Kitunda kwani kwa sasa watu wameanza kujenga na wengine wameanza kulima katika maeneo hayo.
“Sina cha kusema zaidi ya kuipongeza Serikali na Rais wetu Magufuli ila tunaomba muda uliowekwa wa mwisho saa 12 jioni kwa siku uongezwe ili shughuli zingine ziendelee pia tunaomba kivuko hiki kizidi kuboreshwa ili usafiri uwe wa uhakika,” alisema Omary.
Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba tani 50 kimeanza kufanya kazi Machi,2018, kinabeba abiria 100, magari madogo 6 pamoja na magari makubwa mawili kwa kila safari moja na kwa siku kivuko hicho kinakadiriwa kubeba abiria wasiopungua 900.
Kivuko cha MV Kitunda kinachofanya kazi kati ya
kuvusha watu kutoka Lindi mjini hadi Kitunda kikiwa na uwezo wa wa
kubeba mizigo tani 50, abiria 100, magari madogo 6 makubwa mawili
inakadiriwa kwa siku kinabeba abiri 900. Kabla ya uwepo wa Kivuko hiki
wakazi wa Kitunda walikuwa wanatumia mitumbwi kuvuka upande wa pili.
Kivuko hiki kimepelekwa Mkoani Lindi kikitokea Tanga kwa amelekezo ya
Rais Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni kutatua kero ya wakazi wa
Kitunda na maeneo mengine ya Lindi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...