NA MWANDISHI MAALUM - ORCI
TAASISI ya Saratani Ocean Road (ORCI) imefanikiwa kuvuka lengo walikojiwekea kuwachunguza watu 1000 kujua iwapo wana maambukizi ya virusi vya homa ya ini, katika kambi maalum ya uchunguzi iliyofanyika Julai 27 hadi 31, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo leo kueleza tathmini ya kambi hiyo iliyofanyika hospitalini hapo kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kinga ya Saratani ORCI, Crispin Kahesa amesema mwitikio wa watu kujitokeza kuchunguzwa afya zao ulikuwa mzuri.
"Tulipanga kuwachunguza watu 1000 katika siku hizo tano, tumefanikiwa kuwachunguza watu 1197, kati ya hao 49 tumewagundua tayari wana maambukizi ya homa ya ini," amesema.
Amesema watu hao waliokutwa na maambukizi wanaendelea kufanyiwa vipimo zaidi ili waweze kupangiwa aina ya matibabu wanayostahili.
"Mtu akichunguzwa kwa kipimo cha kwanza Screening test, akigundulika ana maambukizi anapimwa tena kwa vipimo vya ziada Confirmatory test, tunaangalia hatua ambayo ugonjwa upo ili tuweze kumpangia matibabu anayostahili," amesema.
Amesema kambi hiyo ilifanykma ili kuenda sambamba na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo 'Tafuta mamilioni ya watu wenye maambukizi ya homa ya ini wasiojulikana'
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...